Waziri wa Kazi na Ajira Mhe. Gaudentia Kabaka leo tarehe 19/09/2013, amezindua rasmi mchakato wa maandalizi ya ushiriki wa Wajasiria mali wa Tanzania katika Maonesho ya 14 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yajulikanayo kama Nguvu kazi/Jua kali.
Maonesho hayo yaliyoanza kufanyika mwaka 1999 jijini Arusha Tanzania wakati wa kusainiwa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yameendelea kufanyika kila mwaka kwa mzunguko katika nchi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Dhumuni kuu la maonesho haya ni kuwezesha sekta isiyo rasmi kukua na kurasimisha shughuli zao katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwapatia fursa Wajasiriamali wa sekta hii kuonesha bidhaa zao, kukutana na wenzao, kubadilishana taarifa, ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na huduma pamoja na kuwezesha kupanuka kibiashara.
Jumla ya Wajasiriamali 1,070 kutoka nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki wanategemewa kushiriki na Tanzania inatarajiwa kupeleka washiriki 250.
Mhe. Waziri Kabaka amesema,ili kurahisisha na kuharakisha ushiriki wa Wajasiriamali wa Tanzania katika maonesho hayo, kuna swala la usajili, na fomu za usajili pamoja na vigezo vya kuangalia kabla ya kujaza fomu ambavyo vinapatikana kwenye Tovuti ya Wizara ambayo ni www.kazi.go.tz
IMETOLEWA
Ridhiwan.M.Wema
Msemaji
WIZARA YA KAZI NA AJIRA.
19/09/2013