Mdau wa maendeleo katika jimbo la kalenga Iringa Bw Jackson Kiswaga kushoto akikabidhi msaada wa madawati 30 yenye thamani ya zaidi ya Tsh milioni 1 kwa mwenyekiti wa kijiji cha Lumuli Bw Mendrady Nywage kwa ajili ya shule ya msingi Lumuli ,kulia ni diwani wa viti maalum tarafa ya Kiponzero Vumilia Mwenda na wa pili kushoto ni diwani wa kata ya Lumuli Charley Lutego pamoja na wajumbe wa serikali ya kijiji hicho
MDAU wa maendeleo katika jimbo la Kalenga mkoa wa Iringa Jackson Kiswaga ametoa msaada wa madawati 30 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1 katika shule ya msingi Lumuli ili kumaliza kero ya madawati shuleni hapo.
Huku akimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu hapa nchini hata kufanikisha mpango wa shule za sekondari za kata ambazo matunda yake yanaonekana kwa kila mmoja.
Akikabidhi msaada huo leo Kiswaga ambae ni makazi wa jimbo hilo la Kalenga alisema kuwa akiwa ni miongoni mwa wakazi wa jimbo la Kalenga ameguswa na jitihada mbali mbali zinazofanywa na wananchi wa jimbo hilo pamoja na mbunge wao Dr Wiliam Mgimwa .
Kwani alisema kuwa mbali ya kazi nzuri inayofanywa na serikali ya chama cha mapinduzi (CCM) chini ya mwenyekiti wake Taifa Rais Dr Jakaya Kikwete bado watanzania wanapaswa kuendelea kutambua utendaji kazi makini wa serikali ya CCM na pale wanapopata nafasi ya kuchangia maendeleo ni vema kuunga mkono jitihada hizo.
" Mimi kama mzaliwa wa kijiji cha Nyamihuu jimbo la Kalenga mbali ya kuwa kwa sasa naishi jijini Dar es Salaam kwa kufanya shughuli zangu za ajira ila bado natambua wazi kuwa bila CCM kuweka misingi mizuri ya maendeleo katika elimu yawezekana leo nisingekuwa hapa nilipo ....hivyo kazi hii nayoifanya leo ni kuunga mkono kazi ya CCM"
Kiswaga alisema kuwa akiwa kama mdau wa maendeleo ataendelea kusaidia jamii ya mkoa wa Iringa kulingana na uwezo wake na kuwataka wakazi wengine wa mkoa wa Iringa kukumbuka kurudi maeneo yao waliyozaliwa na kusaidia shughuli za kimaendeleo zinazoibuliwa na wananchi.
Awali mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lumuli Bw Mendrady Nywage alisema kuwa kijiji hicho kilimwomba Kiswaga kusaidia msaada huo wa madawati pindi alipoalikwa kama mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba shuleni hapo.
Hata hivyo alisema mahitaji halisi ya madawati ni 40 na kuwa tayari Kiswaga ameahidi kusaidia madawati 10 yaliyosalia shuleni hapo na hivyo kumaliza kabisa tatizo la madawati katika shule hiyo ya msingi Lumuli.
Diwani wa kata ya Lumuli Charlesy Lutego mbali ya kumpongeza Kiswaga kwa msaada huo bado alisema katika kata yake kuna changamoto nyingi ikiwemo ya majengo ya shule mbali mbali ya shule kukamilika kujengwa bila kupauliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kutokana na kukosa uwezo wa kununua mbao na bati zaidi ya 400 za kuezekea.