Mwandishi Kenneth John wa matukiodaima.com Dar es Salaam
Taasisi ya wanawake na maendeleo (WAMA) na Management Development For Health (MDH) Tanzania kwa kushirikiana na wizara ya afya na ustawi wa jamii itafanya mkutano wa kitaifa utakaohusu kutokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa watoto .
Akizungumza na waandishi wa habari jijini dar es salaam mkurugenzi wa idara ya uboreshaji afya wa taasisi ya wanawake na maendeleo (WAMA) Dr Sarah Maongezi alisema kuwa Mkutano huo unataraji kufanyika kesho januari 21 ,2014 jijini dar es salaam katika hoteli ya Serena ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mheshimiwa Mama Salma Kikwete , mke wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa Taasisis ya wanawake na maendeleo (WAMA)
Aidha Dr Maongezi ameongeza kuwa mkutano huo utawahusisha wadau mbalimbali kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii , watendaji katika ngazi ya serikali ya mtaa, mashirika yasiyo ya kiserikali,wadau wa maendeleo,wanaoishi na maambukizi ya WU na UKIMWI ,wanataaluma,mashirika ya kidini kwa pamoja wote hao watashiriki ili waweze kutoa uzoefu wao kuhusiana na changamoto na mikakati muhimu katika kufikia mafanikio ya malengo ya mpango wa kitaifa. Pamoja na hayo Dr Maongezi alisema kuwa ujumbe mkuu wa mkutano huo ni
“Kufanya kazi kwa pamoja kufikia lengo la maambukizi sifuri kwa watoto –Timiza wajibu wako”
Naye mratibu wa huduma ya mama na mtoto Dr Mary Mwanyika Sando kutoka Management And Development for Health (MDH) alisema kuwa wamejikita sana katika kuhakikisha watoa huduma za afya wanatoa huduma kulingana na taratibau na miongozo ya wizara ya afya, na hivyo wanajitahidi kutoa msaada ili kuhakikisha wahudumu wa afya wanapata mafunzo ambayo yanaendana na miongozo ya wizara ya afya.
Vilevile Dr Mwanyika amesema kuwa Management And Development For Health (MDH) kwa kushirikiana na (WAMA ) wamelenga kuhakikisha kweli Tanzania bila Ukimwi,bila maambukizi mapya na bila vifo vitokanavyo na ukimwi au unyanyapaa inawezekana na hivyo wamejitahidi kujikita katika mstari wa mbele ili kuhakikisha kinamama pamoja na familia zao wanapata hizo huduma.
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ilianzishwa mwaka 2006 na mheshimiwa mama Salma Kikwete , ni taasisi isiyo ya kiserikali yenye lengo la kuwaendeleza wanawake na wasichana wa kitanzania hasa waliotoka katika mazingira hatarishi , na moja ya malengo ya taasisi ya WAMA ni kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa kike. |