Mtoto Shadraka Mlawa (12) mkazi wa Tagamenda kata ya Ruaha manispaa ya Iringa afariki dunia baada ya kushindwa kuogelea katika mto Ruaha.
Mwandishi wa mtandao huu wa www.matukiodaima.com Diana Bisangao anaripoti kuwa ,Kamanda wa polisi mkoani Iringa Ramadhani Mungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 28 januari majira ya saa 9 kamili Alasiri.
Kamanda Mungi alisema chanzo cha kifo cha mtoto huyo ni kushindwa kuyahimili maji ya mto huo na hivyo kumzidi nguvu.
Na katika tukio lingine mwanamke mmoja jina limehifadhiwa (20) ambaye ni mkazi wa Semtema kata ya Kihesa katika manispaa ya Iringa alibakwa na mtu asiyefahamika na kusababishiwa maumivu sehemu za siri.
Kamanda Mungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kinyama lililotokea mnamo tarehe 28 januari majira ya saa 9 kamili usiku huku chanzo kikiwa ni tamaa ya mwili, ambapo mtuhumiwa aliyefanya tukio hilo bado anatafutwa.
Mbali na matukio hayo mawili ya kusikitisha Kamanda Mungi alisema watu wasiofahamika waliiba pikipiki yenye namba za usajili T 257 CGC ya rangi nyekundu yenye thamani ya shilingi milioni 1.7 ambayo ni mali ya Robert Msafa (24) mkazi wa Frelimo manispaa ya Iringa.
Mungi alisema tukio hilo lilitokea tarehe 28 januari majira ya saa 2 kamili usiku ambapo watuhumiwa hao bado wanatafutwa.