Mwandishi,Kenneth John wa matukiodaima.com Dar anaripoti kuwa ,
Kamati ya michezo ya mei mosi Taifa imesema kuwa michezo ya mei mosi ya mwaka huu 2014 , itakuwepo kama kawaida na inatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 16 hadi 29 kama inavyokuwa miaka ya nyuma.
Hayo yamesemwa na katibu mkuu wa kamati hiyo Award Safari ambapo amesema kuwa imewalazimu kutoa taarifa hiyo kutokana na uongozi wa kamati hiyo umekuwa ukipigiwa simu mara kadhaa na viongozi mbalimbali wa timu huku wakiulizia juu ya michezo hiyo.
Hivyo kamati hiyo inapenda kuziarifu timu zote zinazotarajia kushiriki kwenye michezo hiyo ya mei mosi , kwamba viongozi wawili yaani mwenyekiti na katibu kutoka kwa kila timu tarajiwa shiriki , wanaombwa kuhudhuria mkutano wa maandalizi , utakao fanyika Februari 14 jijini Dar es salaam kwenye ukumbi wa makao makuu ya chama cha wafanyakazi wa sekta ya mtandao wa simu na huduma Tanzania (TEWUTA) yaliyopo mtaa wa simu yaliyotazamana na club maarufu ya Billicanas ambapo mkutano huo utaanza saa 8 mchana.
Aidha Bw, Safari amesema kuwa kamati tayari imeshawasiliana na uongozi wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) , halikadhalika na chama kinachoratibu sherehe za mwaka huu kwa lengo la kutaka kujua ni mkoa upi utakuwa mwenyeji wa sherehe hizo za mei mosi mwaka huu kitaifa .
Hata hivyo kamati imeziomba timu zote zinazotaraji kushiriki kwenye michezo ya mwaka huu kuvuta subira ,wakati jitihada zikiendelea kufanyika za kujua ni mkoa upi utakuwa mwenyeji wa sherehe hizo Kitaifa , na kuongeza kuwa punde kamati itakapo pata taarifa hizo watazitaarifu timu zote mara moja kwa kupitia vyombo vya habari pamoja na barua za mialiko.
Pamoja na hayo Bw, Safari amebainisha michezo ambayo hushindaniwa kwenye michezo hiyo kila mwaka ambapo amesema ni mpira wa miguu, kuvutana kwa kamba, Riadha, Baiskeli,Karata,Drafti sambamba na Bao.
Ikumbukwe kwamba , michezo ya Mei Mosi Taifa ,imekuwa ikishirikisha wanamichezo wafanyakazi kutoka mashirikisho ya michezo ya SHIMMUTA,SHIMIWI,SHIMISEMITA na BAMMATA, ambapo michezo hii imekuwa ikileta hamasa kubwa na burudani hususani katika kipindi cha kuelekea katika sherehe ya Wafanyakazi Duniani yaani “MAY DAY”