Rais wa chama cha walimu Tanzania(CWT)Gratian Mukoba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Feb 7 na miongoni mwa mambo aliyozungumzia ni pamoja na kero na madai ya walimu kwa serikal
.................................................................................
mwandishi Kenneth John wa matukiodaima.com
Suala la elimu ni jambo nyeti sana kwa nchi yoyote inayohitaji maendeleo katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kibiashara , kwani nchi yenye nguvu kazi ya watu wenye elimu nzuri na ya kutosha ya ya fani mbalimbali, ni rahisi pia kwa nchi husuka kupiga hatua ya kimaendelea.
Lakini ni dhahiri kuwa siku za hivi karibuni elimu imekuwa ikishuka kwa kasi na huku fani ya ualimu ikizidi kushuka thamani, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo masuala ya mazingira duni ya kufanyia kazi kwa walimu kuanzia makazi ya kuishi na vitendea kazi pamoja na mishahara hafifu inayoliliwa na kundi kubwa la wadau wa elimu mara kwa mara nchini.
Kwasasa si jambo la kushangaza kumsikia mzazi au mlezi akimweleza kijana wake kuwa endapo akifeli katika mitihani yake atampeleka kusomea ualimu, na mara nyingine utawasikia hata vijana wenyewe wakiwa katika maongezi yao wakisema kuwa mimi ni kifeli tu nitaenda kujisomea ualimu ili nijishikize, hivyo fani hii inaonekana kama ni fani ya watu walioshindwa na kukata tamaa.
Februari 7 mwaka huu Chama cha walimu Tanzania kupitia Rais wa chama hicho Mwl Gratian Mukoba, alikutana na vyombo vya habari na alibainisha mambo kadhaa ambayo yamekuwa yakiendelea kati ya serikali na walimu nchini, mambo ambayo kwa namna moja au nyingine ukiyaangalia kwa umakini yanaweza kuwa yanachangia kudhorotesha elimu yetu nchini,Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na suala la mishahara duni na hafifu, suala ambalo Mukoba katika taarifa yake kwa wanahabari alibainisha kwamba kumekuwa na vikao mbalimbali vya majadiliano ya nyongeza ya mishahara kwa walimu kutokana na maagizo ya mahakama kuu ya Division ya kazi ya mwaka 2012,Ingwaje pamoja na vikao hivyo bado kumekuwa hakuna chochote kilichopatikana na badala yake serikali ilitoa ahadi na kuwaahidi kuwa ifikapo februari mwaka huu majadiliano juu ya masuala ya kuhusu nyongeza za mishahara yatakuwa yamekamilika.
Halikadharika serikali na walimu wamekuwa katika mikwaruzano kuhusiana , na ulipwaji wa malimbikizo ya madeni ya mishahara na yasiyo ya mishahara, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya februari 7 mwaka huu kutoka (CWT) ilibainisha kuwa madai ya walimu kwa serikali yanayohusiana na malimbikizo ya mishahara yanafikia shilingi Bilioni 40. Sasa ukitathimini utagundua hali hii imekuwa ni miongoni mwa sababu inayowakatisha tamaa walimu ya kufundisha kwa moyo, na hivyo kupelekea viwango vya elimu kuzidi kushuka zaidi nchini.
Pamoja na sababu hizo lakini pia suala la upandishwaji wa madaraja kwa walimu limekuwa ni suala linalokatisha tamaa ya kujiendeleza kielimu kwa baadhi ya walimu ,ambapo (CWT) katika taarifa yake ilionekana kuitupia lawama serikali kwa kushindwa kufanya maandalizi mazuri ya mfumo wa upandishwaji wa vyeo kwa walimu yaani (OPRAS).
Hivyo kutokana na changamoto na kero hizo za walimu, ni dhahiri zimekuwa zikiongeza kusababisha kushuka kwa viwango vya elimu nchini,kwani walimu wamekuwa na changamoto nyingi mno, ni ukweli kwamba endapo mazingira ya kazi na malipo yangekuwa yakilipwa kwa wakati husika, na uboreshwaji wa viwango vya mishahara ungefanyika kwa vyovyote vile walimu wangezidi kujituma kufanya kazi yao ya kuelimisha watoto wa kitanzania vizuri .
Hivyo ni vyema serikali ikajaribu kuzitazama changamoto hizo za walimu kwa undani zaidi, na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha tunaokoa elimu yetu inayozidi kushuka siku hadi siku.
Na ikumbukwe kwamba mara ya mwisho Chama cha walimu Tanzania (CWT) kilipokutana na vyombo mbalimbali vya habari nchini, kilitoa msimamo kuwa endapo itafika mwisho mwa mwezi februari hawajapata ufumbuzi wa kero mbalimbali zinazowakabilia basi watakuwa tayari kutangaza mgogoro na serikali,Hivyo ni vyema kabla ya kufikia huko, serikali ikaangalia namna ya kutatua kero hizo kwani waungwana husema “Usipoziba ufa utajenga ukuta” hivyo ni bora kushughulikia mapema kero walizonazo walimu kwa sasa kabla ya mgogoro huo kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu ambao unaweza kupelekea madhara makubwa zaidi katika sekta ya elimu nchini.