Aliyekuwa mgombea udiwani kata ya Nduli Ayub Mwenda akijinadi mbele ya mwenyekiti wake Chadema Taifa Freeman Mbowe,katika uchaguzi huo uliofanyika hivi karibuni mgombea wa CCM alishinda
Wana CCM Nduli wakimpongeza mshindi wa nafasi ya udiwani Bw Mtove ..............................................................................
Mwandishi Kenneth John wa matukiodaima.com Dar
Kituo cha taarifa kwa wananchi (TCIB) kimetoa tathimini ya uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika hivi karibuni sehemu mbalimbali nchini , na kubaini mambo kadha wa kadha katika chaguzi hizo ikiwa ni pamoja na kampeni hizo kukosa busara,
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mkurugenzi mtendaji wa TCIB, Deus Kibamba amesema kuwa vitendo vya ukosefu wa busara wakati wa kampeni ikihusisha maneno ya vijembe,shutuma na fujo za mara kwa mara , pamoja na baadhi ya wafuasi wa vyama kupanda majukwaani na kuwashambulia wagombea pinzani wao kwa kutumia vyeo vyao katika vyama, sambamba na maeneo wanakotoka,Ambapo kibamba amesema hayo yote yanachangia kupoteza dhana nzima ya umuhimu wa kampeni za kistaarabu na inachangia pia kupunguza idadi ya watu wanaohudhuria mikutano ya kampeni.
Kibamba aliendelea kusema kuwa fujo za mara kwa mara zimekuwa zikitokea hasa kipindi cha kuelekea mwishoni mwa mikutano ya kampeni,Ambapo alitolea mfano katika kata za Sombetini, Nyasura na Nduli ambako watu hawakuwa huru kusema wanaunga mkono chama gani kwa kuhofiwa kufanyiwa fujo na hata kuharibiwa mali zao, Na hivyo TCIB kupendekeza adhabu kali ziwe zinatolewa kwa wagombea na mashabiki wanaobainika kuendesha siasa za fujo,matusi,kejeli,na dharau ili kukomesha kampeni chafu.
Aidha Kibamba amesema kuwa kumekuwa na baadhi ya viongozi wa vyama kusikika wakitoa kauli ambazo zina dalili ya kuhamasisha fujo dhidi ya washindani wao.Hivyo kutokana na hali hiyo TCIB imeanza mawasiliano na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa dhidi ya binadamu (ICC) Bi. Fatou Bensouda kwa lengo la kumuomba atume timu ya wataalam wake kuja Tanzania, ili kufanya uchunguzi na tathimini ya awali juu ya matamshi ya hivi karibuni ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na matamshi ya hivi karibuni pia ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ambapo alinukuliwa akiwataka wanachama wa chama chake kuacha unyonge na kuonewa wakati wa uchaguzi na waamke na kujibu mapigo.
Ambapo Kibamba amesema kuwa endapo matamshi kama hayo yakiendelea yanaweza kusababisha fujo kubwa na kupelekea mauaji ya ajabu hususani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Pamoja na hayo Kibamba amesema kuwa kumekuwa na tatizo la mwitikio mdogo wa wapiga kura, tatizo ambalo linaonekana kukua zaidi na kuwa tatizo kubwa, Na kusema kuwa mbaya zaidi baadhi ya vyama vimeonekana kufurahia pindi wanapoona watu wachache zaidi wakijitokeza kupiga kura,Hivyo TCIB imependekeza sheria za uchaguzi zifanyiwe mabadiliko ili kuzuia mshindi kutangazwa mpaka idadi ya wapiga kura inapofikia asilimia hamsini ya wapiga kura walioandikishwa katika eneo husika.
Sambamba na hayo Kibamba amesema kuwa TCIB imesikitishwa na mwitikio mdogo wa upigaji kura pamoja na kuwepo kwa hamasa kubwa inayoonekana wakati wa kampeni.
Na kutokana na hali hiyo TCIB ilitaka kujua tatizo hasa ni nini, na ndipo walibaini kuwa uboreshaji usio wa kudumu na wa mara kwa mara wa daftari la kudumu la wapiga kura umekuwa ni tatizo kubwa linalowakosesha wananchi wengi haki ya kupiga kura hususani vijana waliokuwa na umri wa miaka 17 wakati wa zoezi la uboreshaji wa daftari kwa mara ya mwisho mwaka 2010.
Hivyo TCIB imetoa wito kwa tume ya uchaguzi kuweka utaratibu wa watu kujiandikisha kila mara na sio mara moja kila baada ya miaka mitano.
Halikadharika Kibamba amesema kuwa kutokana na masuala yaliyojitokeza katika tathimini na ufuatiliaji walioufanya wa uchaguzi mdogo wa madiwani,wamegundua ipo haja ya kuimarisha mfumo mzima wa uchaguzi kwa kuweka makatazo juu ya mambo yanayotishia kuharibu uchaguzi, na kuongeza kuwa TCIB ipo tayari kusaidia kuimarisha Jeshi la polisi kwa kuwapeleka kuona jinsi Polisi wa Nchi nyingine wanavyosimamia usalama katika uchaguzi.