Mwandishi Kenneth John wa matukiodaima.com Dar Imebainika kuwa wananchi 7 kati ya 10 wanaamini mtu tajiri hawezi kuadhibiwa kwa uhalifu au kosa alilotenda.
Takwimu hizo zimetolewa jijini Dar es salaam na mtafiti wa asasi ya Twaweza Bw; Evans Mushi alipokuwa akitoa muhtasari wa utafiti wenye jina la “JE, TUKO SALAMA?”ambapo wananchi 6 kati ya 10 ilibainika kuwa wanaamini viongozi wa dini, maafisa wa polisi, viongozi waandamizi wa serikali na viongozi wa umma hawawezi kuadhibiwa kwa makosa au uhalifu wao.
Aidha Mushi amesema kuwa katika tafiti hiyo wananchi walipoulizwa ni kwanini watu hawaripoti uhalifu kwa polisi, Watanzania walionekana kulaumu suala la rushwa na polisi kutowahudumia ipasavyo, ambapo takwimu zilionyesha kuwa Mwananchi mmoja kati ya watano amesema kuwa atalazimika kumlipa polisi kiasi cha pesa ili apatiwe msaada,na huku idadi hiyo hiyo ikisema polisi wasingewasikiliza au kuwajali pindi wanapofikisha taarifa kituoni.
Mushi aliendelea kusema kuwa tafiti hiyo pia ilichunguza mtazamo wa watu kuhusu mfumo wa sheria, ambapo kwa hali ya kawaida watu wanaporipoti uhalifu kwa polisi, ni haki yao kutarajia kuwa polisi watajaribu kumkamata mhalifu na kisha kumfikisha mahakamani na hukumu kutolewa kwa mujibu wa sheria. Lakini hali ilionekana tofauti kwani takwimu zilionyesha kuwa Watanzania wana imani ndogo kama hayo yanatendeka.
Huku nusu yao (52%) wakiamini kama mwananchi wa wakawaida atafanya kosa au uhalifu ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria, jambo lililoashiria kutia shaka, Halikadharika wananchi pia walionekana kuwa na mtazamo wa kutokuwepo kwa usawa mbele ya sheria kulingana na hadhi ya mtu.
Hata hivyo takwimu za tafiti hiyo zilionyesha kuwa wananchi wanapokumbana na uhalifu, wangependa kuripoti polisi, ingawa ni nusu tu ya wananchi wote (47%) wanaofanya hivyo na huku idadi ikionekana kuwa kubwa zaidi mijini ambako watu 6 kati ya 10 (59%) waliripoti kuwa wangeweza kuripoti uhalifu polisi, ikilinganishwa na maeneo ya vijijini ambako watu 4 kati ya 10 (39%) pekee ndiyo wangefanya hivyo. Ingawaje takwimu hizo zinaweza kusababishwa na uwepo wa polisi kwenye maeneo ya mijini kuliko vijijini.
Lakini hata hivyo kwa mujibu wa maafisa watendaji wa vijiji na wenyekiti wa mitaa, vitongoji inaripotiwa kuwa jamii 6 kati ya 10 (62%) haina polisi. Na huku hali ikionyesha kuwa ni nzuri zaidi maeneo ya mijini ambapo mitaa minne kati ya kumi (36%) ndiyo yenye ukosefu wa polisi, Wakati maeneo ya vijijini takribani vijiji 8 kati ya 10 (76%) waliripoti kutokuwa na maofisa wa polisi.
Pamoja na hayo Mushi amesema kuwa takwimu za tafiti hiyo zimeonyesha kuwa vurugu katika jamii hutokea kwa wingi zaidi kuliko wizi, ambapo Februari 19,2014 Dar es salaam karibu nusu (46%) ya watanzania wote wamearifu kuwa wameshawahi kushuhudia vurugu katika jamii ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita, ikilinganishwa na idadi ya mtu mmoja kati ya watano anayeripoti kuwa amewahi kuibiwa kitu na wezi,Na huku nusu ya watanzania wote wanaripoti kuwa hawajawahi kuibiwa kitu, halikadharika watu wanne kati ya kumi ndio hawajawahi kushuhudia vurugu au ghasia katika jamii.
Itakumbukwa kwamba matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wa utafiti wenye jina la Je,Tuko Salama? ambapo wananchi watoa taarifa kuhusu hali ya usalama wa nchi.Na Muhtasari huu ni kwa mujibu wa takwimu kutoka sauti za wananchi, halikadharika utafiti kwa njia ya simu za mikononi wenye uwakilishi wa kitaifa uliofanyika kwenye kaya zote Tanzania Bara.