Hali kama hii inahatarisha usalama wa vyombo hivi wahusika wako wapi kuhakikisha miundombinu inakua vizui ili kuepusha maji kujaa barabarani kiasi hiki
Hii ndiyo hali halisi ilivyokuwa maeneo ya kariakoo barabara ya uhuru ambapo maji yanaonekana kujaa baada ya mvua kunyesha jana na alfajiri ya leo hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji
Hivi ndivyo hali ilivyo barabara ya uhuru kariakoo jijini dar es salaam
Kamera ya mtandao huu ilimnasa dereva boda boda huyu akihangaika kujikwamua katika maji yaliyojaa eneo la kariakoo barabara ya uhuru. Picha na Habari Na Kenneth John wa MATUKIODAIMA.COM, Dar-Es-Salaam
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es salaam kwasasa, kumesababisha baadhi ya barabara za jiji hilo kujaa maji na hivyo kusababisha foleni pamoja na usumbufu kwa watumiaji wa barabara hizo.
Mtandao huu ulifika maeneo ya kariakoo katika barabara ya uhuru karibia na Benki ya akiba na kushuhudia magari,pikipiki,bajaji na maguta halikadharika na watembea kwa miguu wakipata taabu kupita katika eneo hilo lililokuwa limejaa maji, huku baadhi ya madereva wanaoutumia barabara hiyo katika safari zao wakionyeshwa kukerwa na barabara hiyo kutokana na kuwa na mashimo makubwa na hivyo kuwawia vigumu kuyaona mashimo hayo pindi maji yanapokuwa yamejaa, na badala yake hujikuta wakiingia kwenye mashimo hayo na kusababisha kuharibu baadhi ya vifaa vya kwenye magari yao hususani shokapu.
Hata hivyo mtandao huu ulibaini kuwa maji hayo yanajaa kutokana na kutotengenezewa muelekeo mzuri wa kuelekea pamoja na baadhi ya chemba za maji zilizopo maeneo hayo kuonekana kuziba kutokana na kujaa taka za aina mbalimbali ikiwemo mifuko ya plastiki, sambamba na chupa za maji na juice, na hivyo kupelekea maji katika eneo hilo kukosa mahali mahususi pa kuelekea na badala yake kujaa barabarani.
Na kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa uliyotolewa hivi karibuni na mamlaka ya hali ya hewa nchini ilibainisha kuendelea kuwepo kwa mvua katika jiji hilo ,hivyo ni vyema sasa mamlaka husika za jiji hilo kuangalia ni namna gani ya kulitatua suala hili mara moja ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza zaidi ya hayo ya kusababisha uharibifu wa vyombo vya moto.