Hassan Mbomboko |
Secky Kasuga
Mbunge Mchungaji Msigwa
MBIO za Uzalendo za pikipiki kwa ajili ya kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar zachafua hali ya hewa jimbo la Iringa mjini baada ya jumuiya ya umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) kumvaa mbunge mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) kwa kumtaka aonyeshe uzalendo kwa wananchi wa jimbo hilo kwa kukabidhi jimbo hilo kwa chama cha mapinduzi (CCM) kutokana na kushindwa kuwawakilisha vema wananchi.
Pia UVCCM imekishambulia chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) na chama cha wananchi (CUF) kwa kuendelea kushinikiza suala la serikali tatu badala ya mbili ambazo ni mahitaji ya watanzania na kuwa wao kama UVCCM msimamo wao ni kama ni serikali mbili pekee na kushauri bunge la katiba kuvunjwa kutokana na mwelekeo linalokwenda nao kwa sana kuwa si wa kuandaa katiba bora bali ni kuandaa maisha bora kwa wajumbe wa bunge hilo.
Akizungumza jana mjini hapa wakati wa mapokezi ya mbio za pikipiki kutoka mkoa wa Njombe mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UVCCM Taifa Secky Kasuga alisema kuwa mbunge Msigwa mbali ya kuaminiwa na wana Iringa mwaka 2010 na kumchagua kama mbunge wa jimbo hilo ila bado mbunge huyo ameonyesha kutelekeza maendeleo ya jimbo hilo.
" Mbunge Msigwa amefeli kuwawakilisha wana Iringa mjini kutokana na muda mwingi kuzungumzia masuala ya kitaifa na kuacha kuzungumzia maendeleo ya jimbo la Iringa mjini ambalo linakabiliwa na changamoto mbali mbali ...hivyo jimbo hilo hili kwa sasa ni kama mtoto yatima anayeishi kwa kutegemea hisani za majirani "
Kasuga alisema kuwa hivi sasa shughuli za kimaendeleo katika jimbo la Iringa mjini vinafanywa na serikali ya CCM huku mbunge akiendelea kuzungumzia masuala hayo ya kitaifa ambayo pia yana wasemaji wake.
" UVCCM kupitia mkakati wa amsha amsha tumejipanga kuwarejesha vijana wote ambao walikimbilia Chadema ambao sasa wamebaini kuwa chama hicho hakipo kwa ajili ya vijana wala wananchi ila kipo kwa ajili ya viongozi wa juu hivyo lazima sasa atambue hivyo na awe tayari kurejesha jimbo CCM"
Akizungumzia kuhusu bunge la katiba linaloendelea mjini Dodoma Kasuga alisema mbunge hilo limepoteza mwelekeo na kushauri Rais Dr Jakaya Kikwete kulivunja bunge hilo ili kunusuru mabilioni ya shilingi yanayoteketea kwa malumbano yasiyo na tija katika kuunda katiba mpya ,fedha ambazo zingeweza kutumika kuendeleza maendeleo kwa wanachi .
Kwani alisema hadi sasa hakuna jambo la maana ambalo wajumbe hao wa bunge la katiba wamefanya zaidi ya vituko na vioja ambavyo havina faida katika uudaji wa katiba hiyo .
Alisema ukiacha CCM ambacho kilipita kwa wananchi na kukusanya maoni sahihi ya serikali mbili vyama vingine vimeshindwa kufanya hivyo na badala yake kupeleka maoni ya viongozi wao wa juu ambayo hayana faida kwa maslahi ya Taifa .
Hata hivyo alisema kuwa mbali ya vyama vya upinzani kikiwemo chadema mbali ya kuomba katiba mpya ila bado wameonyesha kugawanyika na wengi wao wamefikia kutoa maoni yao binafsi .
Huku kiongozi wa mbio hizo za pikipiki Taifa na mjumbe wa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM kupitia UVCCM mkoa wa Morogoro Hassan Mbomboko alisema wajumbe hao wamepoteza dira kutokana na kujikita zaidi kuelezea suala la serikali tatu na kuacha mambo mengine ya kimsingi .
Kiongozi huyo alisema kuwa lengo la Rais Kikwete kuanzisha mchakato wa katiba mpya lilikuwa ni zuri ila wajumbe hao wameshindwa kutimiza wajibu wa watanzania na badala yake wameonyesha kushindwa kuifanya kazi hiyo na kuendelea kutafuna pesa za watanzania .
Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi Bw Miraji Mtaturu alisema kuwa mbali ya kumheshimu aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji Joseph Warioba ila bado anataka kujua sababu ya kuchakachua maoni ya watanzania na kupachika maoni yake ya serikali tatu .
Mtatura alisema ni vema vyama vya siasa kuacha upotoshaji katika mchakato huo wa katiba na badala yake kuangalia maslahi ya Taifa kwa kuwa na serikali mbili pekee.