Quantcast
Channel: Francis Godwin ::Mzee wa matukio daima::
Viewing all articles
Browse latest Browse all 2596

TAARIFA KWA UMMA TATHMINI YA ASASI ZA KIRAIA JUU YA MWENENDO WA MCHAKATO WAKATIBA MPYA UNAOENDELEA KATIKA BUNGE LA KATIBA TAREHE 17 APRILI 2014 UTANGULIZI

$
0
0

TAARIFA KWA UMMA
TATHMINI YA ASASI ZA KIRAIA JUU YA MWENENDO WA MCHAKATO WAKATIBA MPYA UNAOENDELEA KATIKA BUNGE LA KATIBA TAREHE 17 APRILI 2014
UTANGULIZI
Sisi wana AZAKI tumekubaliana kutoa taarifa na msimamo wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kwa wajumbe wa Bunge Katiba na wananchi kwa ujumla juu ya mwenendo wa mchakato wa kupata katiba mpya unaoendelea sasa mjini Dodoma. Msimamo wetu wa AZAKI umetokana na mikutano kadhaa ya wakuu wa AZAKI mbalimbali uliolenga kutathmini mchakato wa katiba na kuangalia tulikotoka, tulipofikia na huko tuendako. Tathmini ya AZAKI imejikita katika kuangalia zaidi mwenendo wa mchakato wa katiba hasa hatua ya sasa ya mjadala katika Bunge la Katiba na pia hatua inayofuata ya kupitisha katiba pendekezwa kwa njia ya kura ya maoni. Ila katika tamko hili tutazungumzia zaidi mwenendo wa mijadala ya Bunge la Katiba kutokana na uharaka na unyeti wake kwa sasa.
Tamko hili la AZAKI kuhusu mwenendo wa sasa wa Bunge la Katiba umelenga kutoa msimamo wa AZAKI katika mchakato wa Katiba; kushauri na kukemea yale ambayo tumeona yanapelekea kuwakosesha watanzania fursa ya kupata katiba waitakayo na kwa muda muafaka na kwa maridhiano yenye kutanguliza utaifa na kuheshimiana. Tunafahamu kabisa katiba yoyote ile ni lazima ipate uhalali kwa makundi yote katika Taifa ili iweze kutekelezeka. Njia nzuri ya kupata katiba itakayokuwa na sura ya kitaifa ni kuandaa sheria na taratibu shirikishi na kuziheshimu. Kuheshimu ngazi zote za kisheria katika mchakato pamoja na kuzingatia suala la maridhiano ni njia nzuri ya kupata katiba yenye ridhaa ya wananchi wote.
Msimamo wa AZAKI

Sisi wana AZAKI ambao orodha yake imeambatanishwa na tamko hili tunaamini na tunatambua kuwa Katiba ni sheria mama inayotoa mwongozo wa namna gani wananchi wanataka kuendesha mambo ya umma na ustawi wa maisha yao. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndio inatumika sasa (1977) Ibara ya 8(1) (a); "wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi na kwa mujibu wa Katiba…’’.Tofauti na Michakato yote ya kupata katiba iliyokwisha fanyika miaka ya nyuma ,huu ndio mchakato wa kwanza na wa kipekee ambao umetambua na kuyatafuta maoni ya wananchi katika kupata katiba ya nchi yao. 

Kimsingi Mchakato huu ambao ni mwitikio wa madai ya wananchi kwa maika mingi na kuanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete unakidhi matakwa ya hati ya makubaliano ya Muungano kama inavyojieleza katika ibara yake ya saba; nukuu "The President of the united Republic: in agreement with the Vice-President who is head of the Executive in Zanzibar shall- (a) Appoint a Commission to make proposals for a Constitution for 2
the united Republic. (b) Summon a Constituent Assembly composed of Representatives from Tanganyika and from Zanzibar in such numbers as they may determine to meet within one year of the commencement of the union for the purpose of considering the proposals of the Commission aforesaid and to adopt a Constitution for the united Republic". 

Katika mchakato huu, Tume ya mabadiliko ya katiba ilikusanya na kuchambua maoni ya wananchi ambayo yametoa taswira ya kile ambacho wanachi wamesema wanataka kiwemo kwenye katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; jambo ambalo sisi wana AZAKI ambao ni sehemu ya wananchi tunathamini sana mawazo ya wananchi na kazi ya uweledi iliyofanywa na Tume kuyaweka sawa mawazo hayo.

 Kwa mantiki hiyo, ni msimamo wetu kama jamii kuitetea Rasimu ya Pili ambayo kimsingi ndio imebeba maoni ya wananchi yaliyokusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba namba 83. 

Tunasema tunatetea Rasimu ya Pili kwa sababu:-
Hadi sasa hakuna maoni yoyote ambayo kisheria yanapaswa kufanyiwa kazi na Bunge la Katiba zaidi ya yale yaliyomo kwenye Rasimu ya Pili ya katiba. 

Kwa kuwa wananchi waliotoa maoni ndio msingi na chimbuko la madaraka yote na mamlaka ya nchi hii. 

Ni kwa kupitia rasimu hii wananchi wametamka muundo wa uongozi wa Nchi hii, namna ya kuwapata na kuwawajibisha viongozi, halikadhalika ni kupitia rasimu hii wananchi wamegawanya madaraka kwa viongozi wao. 

Aidha, jambo lingine linalotufanya tusimamie na kutetea rasimu hii ya wananchi ni uzito wa hatua za michakato ya awali iliyokwisha pita kabla ya Bunge la Katiba. Kwa mfano katika hatua za msingi za mchakato Bunge maalumu la Katiba limetanguliwa na hatua zifuatazo;
i. Kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Bunge la sasa,
ii. Kuundwa kwa Tume ya Katiba,
iii. Kukusanya maoni ya Watanzania,
iv. Kukusanya maoni ya Wataalum, kufanya uchambuzi wa nyaraka rejea, kufanya tafiti za kina na kuhakikisha kuna ulinganifu wa kisera na kisheria kama Sheria inavyoagiza,
v. Kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine,
vi. Kuchambua na kutathimini maoni ya Wananchi,
vii. Kuandika Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba
viii. Wananchi kujadili na kuboresha Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ngazi ya Serikali za Mitaa yaliyosimamiwa na Tume na Mabaraza yaliyojisimamia yenyewe ya Taasisi za watu wenye malengo yanayofanana,
ix. Kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba Toleo la Pili
3
Hatua zote ambazo zimeshafanyika ndani ya mchakato huu unaonyesha wazi kuwa Bunge la Katiba halipo juu ya mchakato bali ni sehemu tu tena sehemu ni ya pili toka hatua ya mwisho ya Mchakato ambayo itakuwa ni Kura ya maoni.

Toka awali msimamo wa AZAKI umekuwa ni kupatikana kwa katiba ya wananchi yenye malengo mapana kwa manufaa ya nchi na vile vile katiba ya kudumu kwa muda mrefu na wala si katiba ya kusaidia makundi machache katika jamii ya Watanzania tena wakati mwingine kwa malengo ya muda mfupi kabisa. 

Vile vile AZAKI tumekuwa na msimamo kwamba katiba itakayopatikana ijidhihirishe kimuundo kwamba si ya kukidhi maslahi ya watawala bali ioneshe kwamba inatoa majibu ya kero na matatizo yaliyodumu kwa muda mrefu kama vile ufisadi, kutowajibika kwa viongozi na watendaji wa umma, kukosekana kwa maadili ya viongozi, umaskini, ukiukwaji wa haki za binadamu, uchumi mbovu na kero za Muungano. 

Kwa bahati mbaya tumebaini kuwa taswira iliyopo sasa hasa katika Bunge Maalum la Katiba inafifisha matamanio yetu ya Tanzania mpya kwa kuwa haioneshi dalili zozote nzuri za kupata katiba ya wananchi kwa sababu mbalimbali kama zifuatavyo; 

Kwanza, majadiliamo Bungeni yamekosa utashi wa utaifa, umepoteza moyo wa maridhiano na kuheshiminiana, badala yake tunaona ubabe, ubaguzi, vijembe, vitisho, nguvu ya wingi wa watu na vyama. 

Pili, Malumbano yasiyo na tija na yaliyopoteza muda na rasilimali za watanzania. Malumbano hayo ni kama vile ya kura za siri au za wazi wakati siku zote inafahamika kwamba mpiga kura anatakiwa kujengewa mazingira ya kuchagua kile anachokiridhia na wala siyo kwa kumridhisha mtu mwingine. 

Tatu, Mwenendo mzima wa Bunge Maalumu la Katiba kuchukua sura ya ubinafsi na yenye maslahi ya ki vyama zaidi zaidi na kusahau maslahi ya watanzania na mustakabali wa Taifa. 

Nne, Mwenendo wa kusua sua unaotia mashaka kwamba wapo Watanzania wenzetu wasio na nia njema ya kufanikisha katiba mpya kwa muda muafaka na hivyo ucheleweshaji wa makusudi unalenga kufanikisha malengo hayo. Kufanya hivi ni kupoteza rasilimali nyingi za watanzania. 

Tano, Vitendo vya makundi ya wanasiasa kuhoji misimamo na maoni ya baadhi ya wajumbe katika mijadala ya katiba huko bungeni. Kitendo hiki ni kibaya na kinaingilia uhuru wa wajumbe kutoa maoni. Kumekuwepo na vikao vingi vya kisiasa vinavyolenga kuhoji maoni ya wajumbe na pia kuwalazimisha waamue tofauti na mamuzi yao ama ya wananchi. 

Sita, Kumekuwepo na mazingira na kila dalili ya kutaka kulipa Bunge la Katiba madaraka makubwa yasiyostahili ya kutupilia mbali rasimu hii ya wananchi na kuja na rasimu inayopendekezwa na watawala. 

Saba, Kumekuwepo na mazingira ya kila aina ya kuandaa wananchi kupokea katiba pendekezwa iliyotokana na rasimu isiyo ya wananchi kwa kuanza kuwajengea imani kuwa kazi ya Tume ya Katiba haifai na haitekelezeki. 

Kazi hii ya kudharau na kubeza kazi ya Tume na maoni ya wananchi ilianza pale Mhe Rais na Mwenyekiti wa CCM alipolihutubia Bunge na sasa hali hiyo 4
imeendelea kwa kasi ndani ya Bunge la Katiba. Kiwango hiki cha dharau kwa Tume na Maoni ya Wananchi ni kikubwa sana ndani ya Bunge na kinatishia moja kwa moja kupatikana kwa katiba ya wananchi.

Nane, Kumekuwepo na lugha ya vitisho na ubaguzi kwa wananchi na hata kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wenye misimao huru na hasa kwa wale wanaosimama na kutetea maoni ya wananchi. 

Vitisho hivi havitoki tu ndani ya wajumbe wa Bunge la Katiba wenyewe bali hata kutoka kwa viongozi mbalimbali wa nchi. Vitisho hivyo ni pamoja na kauli ya Mhe Rais wakati analihutubia Bunge. 

Mhe Rais aliwaambia wajumbe wa Bunge kuwa kupitisha Muundo wa Muungano ambao wananchi wameupendekeza kwenye rasimu inayojadiliwa Bungeni itatoa mwanya kwa Jeshi litapindua nchi. Kauli hii imeendelea kurudiwa na viongozi mawaziri katika maeneo mbalimbali. 

Waziri William Lukuvi alikaririwa akiwambia waumini wa dini moja mjini Dodoma kuwa endapo mapendekezo ya rasimu inayojadiliwa Bungeni juu ya Muundo wa Muungano yatapita tambueni nchi itatawaliwa na Jeshi.

 Kauli nyingine ya vitisho ni ile inayoelekezwa kwa wajumbe wanaoitetea rasimu hii ya wananchi, wamekuwa wakiambiwa kuwa kupitisha mapendekezo ya rasimu hii, hasa muundo wa shirikisho ni kuvunja muungano na kumrudisha sultani kwa upande wa Zanzibar.

Tisa, Bunge limeanza vibaya kwa kuonyesha ishara mbaya kuwa suala la uwajibikaji na maadili siyo jambo la msingi kwa Tanzania. Hilo tumeligundua maana ya kuona kila kamati na wale waliowengi wakipigia kura mambo ya msingi kwa Taifa kama Tunu za Taifa kwa maana ya "core values". 

Wengi wanapendekeza kuwa uwajibikaji na uadilifu isiwe sehemu ya Tunu za Taifa. Tunapata wasiwasi kuona wabunge hawaoni kama uwajibikaji na uadilifu ni Tunu za Taifa. Hiki ni kiashiria kuwa mambo mengi ya uwajibikaji na uadilifu yaliyowekwa vizuri katika rasimu hii huenda yote yakaondolewa katika sura zinazofuata. 

Kumi, Kumekuwepo na ongezeko la vitendo na matamshi yanayolenga kuichafua Tume ya Katiba kwa malengo binafsi na ya Kisiasa. Kuchafuliwa ama kudhalilishwa kwa Tume ya Katiba, ni sawa na kumdhalilisha Mtanzania aliyetoa maoni yake kwa Tume kama chombo halali cha kisheria katika mchakato wa katiba. 

 Awali Tume ilipaswa kuwa sehemu ya Bunge ila kwa kuwa hawakufuata matakwa ya watawala, Sheria ilibadilishwa na kuweka ukomo wa Tume. 

Hata hivyo, sheria ya mabadiliko ya katiba sura ya 83 Toleo la Mwaka 2014, kifungu cha 31(1) imewekwa bayana kuwa Tume itavunjwa na Rais kwa amri iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali. 

Cha ajabu ni kwamba mazingira ya uvunjwaji wa Tume si tu yametweza hadhi na heshima ya waliokuwa wajumbe wa Tume na watendaji wake lakini yameambatana na matamko ya kebehi na dhihaka kwa watanzania hawa ambao usiku na mchana walifanya kazi kwa uzalendo mkubwa kuhakikisha Rasimu ya Katiba ya wananchi inapatikana ndani ya wakati waliopangiwa kwa mujibu wa sheria.

Kumi na Moja, Tukitambua haki ya kupata habari na ushiriki wa wananchi katika mambo ya msingi ya kitaifa. Wizara ya Sheria imechukua uamuzi wa kuifunga tovuti ya Tume ya mabadiliko ya Katiba. 

Tovuti hiyo imefungwa wakati wananchi wanaitegemea sana kufanya marejeo na kupata taarifa mbalimbali kuhusu uandaaji wa katiba nchini. Si sahihi kusema kuwa, kwa kuwa Tume imevunjwa basi hata na taarifa muhimu za Tume nazo zifungiwe. 

Hapa viongozi wameonesha wazi wazi maslahi binafsi dharau kwa wananchi na chuki dhidi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kitendo cha kuwanyima wananchi na wajumbe wa Bunge la Katiba kupata taarifa za mchakato wa katiba hasa ukusanyaji wa maoni. Tendo hili linapingana na sera za uwazi, ukweli na uwajibikaji na Katiba ya Nchi. Lakini pia ni kiashiria kibaya katika mchakato wa Katiba kwa Kuwa zipo nchi tovuti za Tume zimeendelea kuwepo hadi kufikia utekelezaji wa katiba. 


Kumi na Mbili, Utaratibu uliowekwa kwamba baada ya siku 70 na hata 90 kukamilika umebadilishwa kinyemelea ndani ya sheria ya mabadiliko ya katiba sura ya 83 bila kufuata utaratibu wa kawaida na kumpa mwenyekiti wa Bunge Maalumu uwezo kuomba kibali kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuongezewa siku "kwa kipindi kitakachofaa". 

Hili ni kosa kubwa lisiloleta picha nzuri katika mchakato wa katiba na ni kunyume na misingi ya utawala bora hasa zama hizi za uwazi na ukweli.
Rai yetu Umoja wa AZAKI

i. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 Toleo la 2014, kifungu cha 27(2), Bunge la Katiba na wajumbe wake wanapaswa kuwa huru katika kujadili na kupendekeza katiba mpya. Tunataka kifungu hiki kiheshimiwe na wale wote wanaoingilia uhuru na maoni ya wajumbe wa katiba kuacha mara moja. 

Kama hali ya kuyumbishwa kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa maslahi ya kisiasa halitakoma, basi Bunge hilo haliwezi kutoa katiba yenye maridhiano ya wanajamii wote kama vitisho dhidi ya wajumbe havitakoma. 

Tunavitaka vyama vyote vitambue kuwa hatuundi katiba za vyama bali tunatengeneza katiba ya nchi. Ifahamike kuwa kwa sasa ni vigumu sana kupitisha katiba yenye maelekezo ya chama kama ilivyokuwa mwaka 1977. 

Tutambue kuwa kati ya wananchi million 45 wa nchi, wenye itikadi za vyama hawafiki million 7, hivyo ni kosa kubwa sana kugeuza mjadala wa Bunge La Katiba kuwa ni uwaja wa siasa za vyama badala ya kujadili Katiba. 

ii. Bunge halina mamlaka ya kubadili mambo ya msingi ya katika Rasimu ya Katiba. Bunge linakosa uhalali huo kwanza kutokana na muundo wa mchakato wa uandaaji wa Katiba hapa nchini.

 Muundo wetu umekuwa shirikishi na kuundwa kwa Tume kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi tayari kumelipunguzia Bunge Madaraka makubwa. 

Kwa maana hiyo Bunge hili halina mamlaka ya kubadili rasimu hii zaidi ya kujadili, kuboresha na kuongeza masharti ya mpito. Pili, Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Imeweka bayana kuwa Bunge lina madaraka tu ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba,
6
 
kutunga sheria ya masharti ya mpito, Kanuni za kuendeshea Bunge hilo na masharti yatokanayo. Hivyo kwa mujibu wa sheria hii tayari madaraka ya Bunge hili yamewekewa mipaka na wakitaka kuja na rasimu mbadala nje ya iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba watakuwa wamevunja sheria hii. 

Bunge Maalum linapaswa kuzingatia masharti ya kifungu hiki cha 25 wanapotunga Kanuni za Bunge Maalumu na wanapokuwa wanaendesha mjadala. Wanapaswa kuhakikisha hawatungi kanuni zitakazopingana na kifungu hiki. 

iii. Pamoja na udhaifu huu wa kisheria bado Bunge la Katiba katika mchakato huu halina mamlaka ya kubadili mambo yote ya msingi kama muundo wa Muungano katika rasimu ya katiba.

 Hivyo kwa mujibu wa sheria hii Bunge lina mamlaka kamili ya kujadili na kuboresha rasimu tu na si kutunga rasimu nyingine. Kazi yao ni kupendekeza katiba itakayotiwa muhuri na wananchi kwa kura ya ndiyo. 

Angalizo hili lipo pia katika Hati ya Muungano Ibara ya vii (b), ambayo inasisitiza kuwa Bunge La Katiba litajadili na kupendekeza katiba kwa kuzingatia pendekezo la rasimu ya Tume.
iv. Katika taifa lolote lile msingi wa uendeshaji wa Taifa hutegemea sana sheria Kuu Katiba (Supreme Law). Katiba huainisha Tunu "core values" na misingi ya nchi yoyote, pia hutoa migawanyo na ukomo wa madaraka na majukumu mbalimbali ya mihimili mikuu ya dola.

 Kutokana na umuhimu huu mchakato wa katiba ni lazima uwe shirikishi katika ngazi zote likiwemo hili la Bunge la Katiba. 

Katiba inapaswa kuakisi mambo ya wananchi ili kuifanya waimiliki na kuiheshimu katiba hiyo. Ukiwa na Katiba ambayo wananchi hawakushiriki vizuri, lazima Katiba hiyo itakuwa vigumu kupata utekelezaji na umiliki wa wananchi. 

Kitendo cha Bunge la Katiba kujitwalia madaraka wasiyokuwa nayo na kutupilia mbali misingi mikuu ya kikatiba iliyopo katika rasimu ya pili ni sawa na kuwaweka wananchi nje ya mchakato huu. Na kwa maana hiyo kama wananchi watawekwa nje ya mchakato huu kwa kutupilia mbali maoni yao ni dhahiri katiba itakayopendekezwa itakuwa imekosa uhalali wa kisheria na kimaadili. 

v. Bunge la Katiba si chombo cha uwakilishi na pia hakina maamuzi ya mwisho. Uwepo wa kura za maoni hueleza wazi wazi kuwa Umuhimu wa kura za maoni ni kwa ajili ya kuhakiki kama mawazo ya wananchi kama yamezingatiwa na Bunge la Katiba na hatua zingine. 

Kwa utaratibu huu inakuwa ni vigumu kusema Bunge la Katiba lina madaraka kuja na katiba ambayo ni tofouti na rasimu ya wananchi. Kama Bunge la katiba lingekuwa chombo cha uwakilishi tusingekuwa na haja ya kupiga kura za maoni kwani wale ni wawakilishi wetu. Hivyo basi Bunge la Katiba siyo chombo cha uwakilishi kwa kuwa hawakupigiwa kura na wananchi, bali ni chombo ambacho ni sehemu ya mchakato wa katiba na kinapaswa kuheshimu na kuzingatia uwepo wa vyombo vingine vya mchakato wa katiba kama Tume na Kura ya maoni. 

vi. Tunawasihi wajumbe sikivu na wenye utaifa na uzalendo wa Bunge hilo la Katiba kusimama kidete bila kujali uchache wao, kutetea maoni ya wananchi katika rasimu ya pili ya katiba.
7
 
Tunawaahidi kuwaunga mkono katika kutetea maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya pili ya katiba.

vii. Tunamwomba mwenyekiti wa Bunge la Katiba, achukue hatua zaidi kwa wale wanaotoa vitisho, matusi na lugha za ubaguzi kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba na watanzania kwa ujumla. 

Kuna watu wamefikia hatua kusema kupitisha mapendekezo ya wananchi ya muundo wa serikali ya Muungano ni kupelekea nchi kumwaga damu na kuchukuliwa na Jeshi. Kauli hizi zikome kwa kuwa zinalenga kuwajaza hofu siyo wabunge pekee bali watanzania wote ili wakubaliana na matakwa yao. 


viii. Tunawasihi wajumbe wa Bunge la Katiba kuacha kubeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwani waliotoa maoni ni sisi wananchi na siyo wajumbe wa Tume. 

ix. Tunawaomba wabunge wa Bunge la Katiba kutumia busara kama ile ilyotumika mwaka 1977 na wajumbe wa Bunge la Katiba la wakati huo, kuridhia ombi la aliyekuwa Waziri Mkuu Marehemu Edward Sokoine kupitisha bila kupingwa rasimu ilyopendekezwa na Kamati Kuu ya Chama. Na sisi Wana AZAKI tunawaomba wajumbe, kwa kuzingatia kuwa wananchi ndio wenye mamlaka ya mwisho wapitishe maoni yao kwa kuyaboresha zaidi na siyo kuyatupa.
Mwisho

Msimamo huu wa AZAKI umezingatia mambo mengi ikiwa ni pamoja na gharama zinazoendelea kutumika, amani, utaifa, umoja, matamanio na shauku ya Watanzania ya kupata katiba mpya na mambo mengine kadhaa. Tunasikitishwa kwamba mjadala unaoendelea kule Bungeni unaondoa matumaini hayo na mbaya zaidi linazidi kuwatenganisha Watanzania badala ya kuwaunganisha kama ilivyotarajiwa. Msimamo wetu wa kuwataka wajumbe wa Bunge kuheshimu maoni ya wananchi utasaidia wajumbe wahame kwenye mtazamo wa kisiasa na kuwa kitu kimoja katika kuafikiana mambo ya msingi ya kujenga taifa kwa vizazi vijavyo.

Tamko hili limeletwa kwenu na umoja wa AZAKI mbalimbali kama zilivyoorodheshwa hapo chini. Umoja huu chini ya Baraza la Taifa la Asasi Zisizo za Kiserikali unajumla ya Asasi Zisizokuwa za Kiserikali zaidi ya 5000 na unajumuisha Mitandao mbalimbali za AZAKI kama vile Jukwaa la Katiba, Mtandao wa Mashirika yanayotoa Msaada wa Kisheria (TANLAP), Policy Forum, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Umoja wa Wanasheria Wanawake Tanzania( TAWLA), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Umoja wa Vyombo vya Habari Kusini Mwa Africa (Misa-Tan), Shirikisho la vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Chama cha walimu Tanzania (CWT), TUCTA, Chama cha Wanasheria Tanzanaia (TLS) etc. 

TATHMINI HII IMELETWA KWENU NA AZAKI KUTOKA TANZANIA BARA NA VISIWANI ZINAZOUNDA UMOJA WA AZAKI UNAOTETEA RASIMU KATIBA YA WANANCHI


--
ONESMO PAUL KASALE OLENGURUMWA
COORDINATOR OF THE THRD-COALITION
P.O.BOX 105926,DAR ES SALAAM,TANZANIA.
TEL +25522 2773038/48
FAX +255 222773037
mobile +255 717-082228/08783-172394

Viewing all articles
Browse latest Browse all 2596

Trending Articles