Na Esther Macha, Mbeya
WAZEE wanaoishi katika Kata ya Mshewe Wilaya ya Mbeya Vijijini wamesema kuwa kutokana na kutopata huduma za matibabu katika Zahanati zilizopo kijijini hapo wanalazimika kutumia dawa za miti shamba ili waweze kupona maradhi mbali mbali yanayowasumbua.
Mwito huo umetolewa juzi na wazee wa Kijiji cha Njelenje Kata ya Mshewe wakati walipofanya mahojiano na Mtandao kuhusiana na changamoto ambazo wanazipata katika kupata huduma katika Zahanati hizo .
Mmoja wa wazee wa kijiji hicho Solomon Sanga (87)alisema kuwa huduma kwa wazee zimekuwa shida sana kiasi kwamba hulazimika kwenda kutafuta miti shamba maporini ili waweze kujitibu.
“Tunalazimika kutumia dawa za miti shamba kutokana na huduma mbaya tunazopata hospitalini, tunaona bora tutumie miti shamba kuliko kwenda hospitali maana hata ukienda hospitali hakuna huduma yeyote tunayopoata zaidi ya wahudumu wa afya kudai tunawasumbua”alisema Mzee Solomon.
Mzee mwingine Bi.Ena Mgata alisema kuwa katika kupatiwa huduma waganga wengine hudai kuwa wakanunue wakati huduma kwa sisi wazee tunajua tunapatiwa bure.
“Hali ilivyo hivi sasa ni heli ya kipindi cha mkoloni tu kwani hata ukiumwa jino unaambiwa utoe sh.10000 ili utoe jino sasa kweli sisi wazee tutakwenda wapi kwa hali kama hii, serikali ilishasema wazee tupatiwe huduma bure lakini hakuna chochote zaidi ya kuteseka tu tukifika hospitali, tunaona bora tutumie dawa za miti shamba tu maana hoispitali zenyewe ndo hizi ”alisema.
Hata hivyo Bw. Solomon alishauri kuwa Katiba ijaayo iwajali wazee na iseme wazi kuwa wanatakiwa kupata huduma bur za matibabu .
Akizungumzia kipengele cha nafasi za uongozi kwa wabunge alisema Katiba mpya kuwepo na muda maalamu wa viongozi kwani wakishachaguliwa wanajisahau na kupotea , wanakuja kipindsi cha kuomba kura tu baada ya hapo wanatekelezwa .
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Njelenje Emmanuel Kalimoja alisema kuwa yeye kama kiongozi hajaweza kupata malalamiko hayo kutoka kwa wazee hao na kuhaidi kulifanyia kazi.