Dr. Owdenburg Moses Mdegela
ASKOFU wa Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa Dr Owdenburg Mdegella amesema kuwa iwapo katiba mpya itabariki kuwa na serikali tatu atalia kwa uchungu kwani wazo la kuwa na serikali tatu ni mzigo kwa Taifa .
Alisema kuwa nchi leo haitawaliki kutokana na kushindwa kukubaliana kama nchi na hivyo wanafikiri kuwa na serikali tatu ni jibu la ufumbuzi wa mambo yao.
Hivyo kuwataka viongozi kuwa makini zaidi na suala hili kwani wapo wanaotaka kufanikisha mambo yao kupitia serikali tatu na kuwa hata kama Muungano hautakuwepo ila katika mambo ya msingi kama Bahari ni lazima hapo kukawa na Muungano kwani haiwezekani ikawa nchi bila kuwa na bahari itafika mahali watasema hata gesi ya Mtwara iliyopo chini ya bahari ni yao .
Japo alisema kuwa rasilimali za Taifa zinawezekana kuweka mipaka mfano zilizopo umbali fulani kutoka Zanzibar ni zao na kutoka umbali fulani kutoka bara ni za watu wa bara.
Askofu Dr Mdegella aliyasema hayo leo alipozungumza na wanahabari kuhusiana na maoni yake katika mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Kwa sasa tunapaswa kuanza na serikali mbili ambazo marais wapeane zamu ya kuongoza mambo ya Muungano pia kuwe na bunge la Muungano pamoja na mawaziri wa Muungano"
Wakati huo huo askofu Dr Mdegella alisema kuwa hapingani na taarifa zilizotolewa na usalama wa Taifa kwa Rais Dr Jakaya Kikwete kuwa wapo baadhi ya viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara ya uuzaji wa madawa ya kulevya.
Alisema kuwa chanzo cha viongozi wa dini kujiingiza katika biashara za madawa ya kulevya ni kutokana na kuwepo kwa kundi la baadhi ya viongozi wa dini wapenda pesa hivyo wanaingia katika biashara za madawa ya kulevya ili kujipatia fedha haramu za kuuza madawa ya kulevya .
" Hata Yesu Kristo alisema kuwa kuna wachungaji wachungaji wamevaa ngozi ya kondoo kumbe ni mbwa mwitu....mimi siwezi kukataa wapo japo siwajui ...ninavyoona wanavyotafuta pesa kiujanja ujanja na mazingira ya ajabu kwa kufanya mazingaombwe na kusema miujiza ...kama wanamdanganya Mungu watashindwa kuidanganya serikali ....lakini la pili la mhimu sana lazima tukubaliane kimsingi wanaohusika na biashara za madawa ya kulevya ni viongozi wenye majina makubwa wapo "
Askofu Dr Mdegella alisema kuwa haiwezekani na haitakuja wezekana kilo zaidi ya 100 zipite katika uwanja wa ndege kwenda nje bila kujulikana na haiwezekani kila wakati Taifa linachafuliwa na biashara ya madawa ya kulevya na ulinzi katika viwanja vya ndege umeboreshwa ila bado watanzania wanakamatwa nje ya nchi na dawa za kulevya wakitokea Tanzania .
Hata hivyo alisema kuwa yawezekana kabisa mtandao wa madawa ya kulevya unahusisha vigogo wa hapa nchini na nchi za nje na kuwa iwapo taswira iliyopo sasa katika Taifa ya biashara za dawa za kulevya ingejulikana kabla ya ziara ya Rais wa Marekani yawezekana asingekubali kufanya ziara katika nchi inayoongoza kwa watu watu kukamatwa na madawa ya kulevya nje
.
Hata hivyo Askofu Dr Mdegella aliwashukia wahubiri wanaoibukia katika maeneo mbali mbali ya nchi na kujipachika vyeo vya uaskofu ,unabii pamoja na baadhi yao kudanganya hata kiwango chao cha elimu na kujiita wao ni madaktari huku wakitambua wazi hawajasoma popote zaidi ya kujifungia ndani na waumini wao na kujipa udaktari .
Tazama video yake katika Youtube(andika Askofu Dr Mdegella atoa maoni yake)