MBUNGE wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe aitahadharisha serikali kuwa vurugu gesi Mtwara hapendi zitokee wilaya ya Ludewa mkoani Njombe katika miradi ya Liganga na mchuchuma.
Alisema kuwa miradi hiyo ya Liganga na mchuchuma haitakuwa na faida kwa wana Ludewa iwapo haitawanufaisha vijana wa Ludewa katika ajira .
“Lazima manufaa ya miradi hii ianze katika wilaya ya Ludewa na vurugu zilizotokea Mtwara kamwe sitapenda kutokea katika wilaya ya Ludewa katika miradi hii”
Mbunge Filikunjombe alitoa kauli hiyo leo wakati akikabidhi vyeti na leseni kwa wahitimu wa mafunzo ya udereva wa boda boda na magari katika kata ya Mndindi na Madope wilaya ya Ludewa .
Alisema kuwa lengo la miradi hiyo ni kulinufaisha Taifa kwa ujumla ila lazima wakazi wa wilaya ya Ludewa wakawa wa kwanza kunufaika na miradi hiyo kwa kupata ajira .
Kwani alisema kuwa hadi sasa jitihada za serikali zimeanzwa kuonekana katika wilaya ya Ludewa kwa kuanza ujenzi wa lami katika barabara ya Ludewa – Njombe ambapo ni mwanzo wa wana Ludewa kuanza kufaidi matunda ya Uhuru baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru wilaya hiyo ya Ludewa haijapata kuwa na lami .
Pia alipongeza jitihada za serikali kuanza mchakato ujenzi wa chuo cha ufundi stadi (VETA) na kuwa chuo hicho kitakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wana Ludewa na hata kuwapata vijana wenye ujuzi wa kufanya kazi katika miradi ya Liganga na mchuchuma.
Mbunge huyo aliwataka viongozi wa jeshi la polisi na serikali ya wilaya ya Ludewa na mkoa kwa ujumla kutambua kazi kubwa ya VETA ambayo wameitoa katika wilaya ya Ludewa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii.
Alisema kuwa upande wa madereva boda boda wanapaswa kuepusha ajali zinazozuilika kwa kuzingatia sheria za barabarani kwani alisema wahitimu wa mafunzo hayo zaidi ya 300 ni ukombozi na kinga ya ajali kwa wahitimu hao.
Mbunge huyo alisema hadi sasa anashangazwa na madereva boda boda kijiji cha Amani ambacho kinaongoza kwa idadi kubwa ya pikipiki ila katika mafunzo wameshindwa kujitokeza .
“Lazima mliohitimu mafunzo hayo kuanzisha umoja wenu ili kuwa kitu kimoja na pindi mtakapoitisha mkutano wa kwanza mimi nitafika kushiriki katika mkutano huo.”
Alisema iwapo wataanzisha umoja wao kamwe hawatatoa rushwa kwa askari wa usalama barabarani na badala yake fedha hizo zitatumika katika shughuli za kijamii kwa kusaidiana kuuguzana ama kusomesha familia .
“Mimi nitakuwa mlezi wa umoja huo wa boda boda katika wilaya ya Ludewa iwapo mtaanzisha umoja huo ikiwa ni panmoja na kuwawezesha zaidi ……..Kumbukeni kuutumia umoja huo kwa kuonyanya wenyewe kwa wenyewe pale ambapo tutaona mwenzetu kati yetu anakwenda kinyume na sheria za usalama wa barabarani.”
Alisema kwa kuwa bado anautamani ubunge mwaka 2015 hivyo iwapo vijana wengi madereva boda boda watakuwa walemavu na kulazwa hospital ama kupoteza maisha kwa ajili za boda boda idadi ya watu wa kumpigia kura itapungua pia
“Ndugu zangu wana mndindi kuweni makini katika kuepuka ajali za barabarani pamoja na kuonynya wenyewe kwa wenyewe mimi naamini heshima ambayo ninatapa nje na bungeni si yangu ni ya wananchi wa jimbo la Ludewa”
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa VETA kanda ya nyanda za juu Veronica Mbele alipongeza jitihada za mbunge huyo katika kuwasaidia wananchi wake hata kuandaa mafunzo hayo kwa madereva .
Alisema kuwa VETA itaendelea kutoa mafunzo ya aina mbali mbali katika wilaya ya Ludewa na mikoa ya Iringa , Njombe na Ruvuma na kuwa moja kati ya mkakati wa VETA ni kujenga chuo Ludewa chuo ambacho kitazalisha watenda kazi wengi ambao watapata ajira katika miradi ya Liganga na mchuchuma.
Bi Mbele alisema sanjari na mafunzo ya udereva VETA wamekuwa wakitoa mafunzo ya utegenezaji sabubu ,batiki, ufugaji wa kuku za kienyeji na shughuli mbali mbali zinazowakomboa wananchi.
MWISHO