Barua iliyonaswa baada ya ofisa mtendaji kuwaandikia wazazi na walezi wa wanafunzi kwa ajili ya kutoa michango. |
=======================================================
Na Gustav Chahe, Kilolo
BAADHI ya wanafunzi wa darasa la saba wakiwemo watoto yatima wa shule ya Msingi Kimala Kata ya Kimala Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa huenda wasifanye mitihani ya mwisho kutokana na kukosa michango ya shilingi 47,000/= ambayo wanadaiwa shuleni hapo.
Baadhi ya wanafunzi hao wameuambia mtandao huu kuwa uwezekano wa kutokufanya mitihani upo kutokana na sababu nyingi ambazo wanaziona ikiwemo ya kutokuruhusiwa kuingia madarasani wakati wa vipindi na madala yake kufanyishwa kazi nje.
Wakiongea na mtandao huu shuleni hapo, wanafunzi hao (majina tunayo) walisema wamekuwa wakifanyishwa kazi na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ahamed Twalipo badala ya kusoma kwa sababu ya kuwa hawajalipa michango.
Walifafanua kuwa licha ya kutokuingia darasani kusoma walizuiliwa kufanya mitihani ya kanda jambo ambalo wananchi walilipigia kelele na kulazimishwa kufanyishwa mitihani 7 kwa siku 2 ambapo walikuwa wakifanya hadi usiku.
Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti, wananchi wa kijiji hicho walisema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amekuwa mbabe kutaka kila anachokitaka yeye kifanyike pasipo makubaliano ya wazazi ama kamati ya shule.
Imeelezwa kuwa miongoni mwa michango hiyo ni pamoja na mshahara wa mratibu elimu ambao mwalimu huyo kwa kushirikiana na ofisi ya kijiji wamebuni licha ya kuwa mratibu huyo analipwa na serikali.
Boniface Kasuga ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya shule hiyo ameonesha kushangazwa na mchango huo kuwa ni mipango ya watu binafsi na kuwa haujawahi kujadiliwa katika mikutano au vikao vya kamati ili kuona umuhimu wa wazazi au walezi kutoa michango hiyo.
“Hii michango ni ya uonezi. Mimi ni mzazi pia lakini mchango huo siujui pamoja na kuwa ni mjumbe wa kamati. Ninachojiuliza ni kwamba; mratibu anateuliwa na Mkurugenzi, kwa nini sisi wananchi tumlipe?
“Pia mchango wa darasa la saba unakujaje kwa kila mwanafunzi kutozwa shilingi 47,000/=? Kuna watu wachache tu ambao wanapanga michango hiyo kama ulaji kwao” alisema Kasuga.
Pia wananchi wamemlalamikia mwalimu huyo kutumia lugha za matusi, kejeli na vitisho kwa wazazi wanaofika shuleni hapo kujiuliza uhalali wa michango hiyo na mara nyingine kuwadharirisha wazazi mbele ya watoto wao shuleni hapo.
Mwalimu Twalipo anadaiwa kuuza chakula walichochanga wananchi kwa ajili ya wanafunzi wawapo shuleni hapo mchana kwa madai ya kukarabati nyumba za walimu bila kushirikisha kamati ya shule.
Mwanafunzi ambaye aliomba jina lisiandikwe mtandaoni alieleza kuwa mzazi wake alidharirishwa na mwalimu huyo shuleni hapo alipofika kutaka ufafanuzi wa michango hiyo ambapo mwalimu Mkuu alimtolea maneno ya dharau, matusi na kumrushia fedha aliyokuwa ameitoa kwa ajili ya mchango ambao amekuwa akirudishwa mara kwa mara kwenda kuuchukua nyumbani.
Fened Ngusulu na Omari Kahemela ni miongoni mwa wananchi walioueleza mtandao huu kwa nyakati tofauti kuwa walitukanwa na kutolea maneno ya matusi na mwalimu huyo shuleni hapo walipofika kwa ajili ya kujua zaidi kuhusu michango hiyo.
Katika mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita uliofanyika kijijini hapo Agosti 28, 2013 alisema kuwa shule za msingi hazina michango na kwamba kama michango hiyo ipo ni makosa.
Mweyekiti wa kamati ya shule hiyo Telaki Ndenga amethibitisha kuwepo kwa michango hiyo na kwamba kamati ya shule haijawahi kushirikishwa juu ya michango hiyo.
“Ni kweli michango hiyo ipo lakini sisi viongozi wa kamati hatuijui wala hatuwezi kuizungumzia. Hiyo ni mipango ya mwalimu mkuu na viongozi wa kijiji ambao wanataka kuila ila ingekuwa halali tungeshirikishwa. Kwa kawaida michango yote halali ambayo inatakiwa kutolewa huwa inajadiliwa kwenye vikao vya kamati kwanza kabla ya kuwatangazia wananchi.
“Cha kushangaza mwalimu Mkuuamegeuza shule kuwa mali yake wakisaidiana na uongozi wa kijiji kuwakandamiza wananchi. Huo ni wizi tu ambao wanaufanya kwa maslahi yao binafsi. Kibaya zaidi wanafanya bila kutushirikisha viongozi wa kamati” alisema.
Hata hivyo barua iliyoandikwa na ofisa mtendaji wa kijiji hicho Festo Mtenga kuwataka wazi na walezi wa wanafunzi wanaodaiwa michango shuleni hapo kutoa haraka vinginevyo hatua kali zitachukuliwa imenaswa na mtandao huu.
Mkuu wa shule hiyo alipotafutwa shuleni hapo kwa ajili ya ufafanuzi zaidi, hakuweza kupatikana kwa kile kilichoelezwa kuwa amekwenda kwenye kikao cha halmashauri wilayani na hata alipopigiwa simu ilipokelewa na mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mke wake na kusema kuwa mumewe hayupo na isingekuwa rahisi kumuona.
Mitihani ya darasa la saba inatarajiwa kuanza kufanyika nchini Septemba 12, mwaka huu.