KATIKA hali isiyo ya kawaida mwanaume mmoja mkazi wa mtaa wa Pangani kata ya Makorongoni katika Manispaa ya Iringa Hamis Said maarufu kwa jina la Mwarabu amemuua kinyama mtoto Raymond Ben Mangungu (2) kutoka na ugomvi wa kimapenzi kati yake na mama wa mtoto huyo ambae kwake ni mpenzi wake .
Imedaiwa kuwa mtuhumiwa huyo wa mauwaji ya mtoto huyo alikuwa amelewa pombe kupita kiasi na si mara ya kwanza kulewa kiasi hicho na kutishia kufanya mauwaji dhidi ya mtoto huyo wa kambo kwa kile alichokuwa akidai kuwa ni fedhea kwake kuishi na mwanamke ambae ana watoto wawili ambao si damu yake.
Wakizungumzia juu ya tukio hilo mashuhuda wa tukio hilo kwa sharti la kutotaja majina yao walisema kuwa imekuwa ni kawaida kwa Mwarabu kumpiga mwanamke huyo na familia yake kwa madai kuwa hataki kuwaona watoto hao wakiendelea kuishi katika nyumba hiyo ambayo ameipanga yeye .
" Huyu bwana Mwarabu alikuwa akifanya kazi ya kuuza korosho mitaani na akirudi usiku amekuwa mkali kwa mwanamke huyo ambae alikuwa akidai kuwa bado amekuwa na mahusiano na baba wa watoto hao wawili .....hata hivyo sisi kama majirani tumekuwa tukishindwa kuwaamua kutokana na mwanaume kuwa na tabia ya kulewa pombe kupita kiasi na hata tukio hili tulijua ni kawaida yao "
Mtoto Tinito Mangungu (6) ambae ni kaka na marehemu alisema kuwa baba yao huyo mdogo alifika usiku na kuwataka wote kuamka kitandani na kuwa hakuna mtu atakayelala katika chumba hicho kama si damu yake.
"Baba mdogo (Mwarabu) alirudi usiku akiwa amelewa na kusema hakuna mtu kulala kitandani na kuanza kumpiga mama kwa meza na viti huku sisi tukilia kumtaka asimpige mama yetu....baada ya hapo alimchukua mdogo wangu na kuanza kumkaba shingo na kumwacha kitandani akiwa amelama bila kuamka hadi sasa mama anasema amekufa"
Akielezea juu ya mkasa huo uliosababisha mauwaji ya mtoto Raymond mama mzazi wa mtoto huyo Bi Kudra Kahemela (23) alisema kuwa kwa upande wake baada ya kutishiwa kuuwawa kwa kipigo alifanikiwa kukimbia katika chumba hicho na kwenda kujificha nje na baada ya muda mwanaume huyo alianza kutapika na pale alipoingia kutana kumsaidia ndipo alipopigwa na kuamua kukimbia kwenda kulala nje ya nyumba hiyo kwa kujiegesha katika nguzo ya umeme iliyopo nyumba ya pili karibu na nyumba ya shekhe wa mkoa Juma Alli Tagalile
Alisema kuwa asubuhi aliingia katika chumba hicho baada ya mwanaume huyo kutoka kwenda katika kilabu cha pombe za kienyeji cha Tulivu kuendelea kunywa pombe na kumkuta mtoto huyo akiwa amelala bila kutikisika .
" Mimi nilijua kama mtoto amelala tu ama amezimia ila baada ya kuwaita watu wazima akiwemo mama yangu mzazi ndipo nilipobaini kuwa mtoto wangu Ray amefariki dunia na ndipo nilipomfuata na kumweleza juu ya tukio hilo ila bado aliendelea kunywa pombe na kudai kuwa mtoto huyo amezimia kwa kelele za usiku ."
Alisema baada ya hapo mwanaume huyo alikimbia hadi Ilala kwa wakwe zake na kuomba msamaha na kusuluhishwa ugomvi wao ila wakati mtengo wa kukamatwa ukiwekwa ndipo alipokimbia kusiko julikana.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia mtoto huyo akiwa amekufa katika kitanda cha wazazi wake huku chini ya chumba hicho thamani mbali mbali pamoja na vyombo vikiwa vimevunjika kutokana na ugomvi huo .
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo wa Pangani kata ya Makorongini Bw Salum Kibaya amethibitisha juu ya kifo cha mtoto huyo na kuwa baada ya tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa kuamkia leo jumamosi Desemba 14 mwaka huu alilazimika kwenda kituo cha polisi cha stendi kuu ya mabasi yaendeyo mikoani na kuwajulisha juu ya tukio hilo na kufika eneo la tukio .
Bw Kibaya alithibitisha pia kuwa ugomvi kati ya wapenzi hao si wa kwanza kutokea japo kwa maelezo ya mwanamke huyo alikuwa mbioni kuolewa na mwanaume huyo na hivyo kuwa na wanaume wawili akiwemo mzazi mwenzake ambae kwa sasa anaishi eneo la Don Bosco mjini hapa.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa huku jeshi la polisi likiwahoji mama wa mtoto huyo ,kama wa mtuhumiwa wa mauwaji hayo ambae ni mkazi wa Mlandizi Kibaha Jijini Dar es Salaam na mama mzazi wa mtoto aliyepoteza maisha.
|