Meneja wa TRA Iringa |
WAFANYABIASHARA mkoani Iringa wafanya mgomo baridi wa kufungua maduka yao huku wakipita mitaani kuwafanyia vurugu wenzao wanaogoma kufunga maduka yao kama sehemu ya hatua ya kuishinikiza serikali kuachana na kuwalazimisha kununua mashine za kodi za kielektroniki (EFD)
Hatua hiyo imepelekea serikali mkoa wa Iringa ikitoa onyo kali kwa kikundi cha wafanyabiashara wanaowafanyia fujo wengine na kuliagiza jeshi la polisi kuwakamata .
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Christine Ishengoma alisema wamepata taarifa ya kuwepo kwa kikundi cha watu wachache ambao wanawafanyia vurugu wenzao ambao wanataka kufungua maduka hayo na tayari msako mkali umeanza toka leo ili kuwakamata watu hao.
“ mimi ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama pia mkoa hivyo sitapenda kuona amani inavurugwa na wachache ….pia tutambue wapo wenye mikopo; kwa faida yao, ya jamii na kwa maendeleo ya mkoa wa Iringa naomba warudi kwenye biashara wakati serikali ikichukua kilio chao na kukifanyia kazi,” alisema.
Taarifa za wafanyabishara hao ya kufunga maduka yao mpaka pale serikali itakapositisha matumizi ya mashine hizo, ilianza kuenea jana kwa kupitia mitandao ya simu na taarifa kutoka kwa kikundi kinachoendesha kampeni hiyo.
Biashara pekee zilizokuwa zikiendelea kwa jana ni zile za vyakula katika masoko mbalimbali ya mjini Iringa.
Huku maduka ya nguo nay ale ya vifaa mbali mbali yalionekana kufungwa huku bar na maeneo ya soko na vyakula ndio yalionekana kufanya kazi .
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Iringa, Lucas Mwakabungu alisema wamepanga kukutana na wafanyabiashara hao saa tisa mchana wa huu ili kuwashauri wasiendelee na mgomo.
“Tunachukua kero yao na tunawaahidi tutakaa meza ya pamoja na serikali ili tufikie muafaka; mfanyabishara nayajua umuhimu wa mzunguko wa fedha yake hatakiwa kupoteza mapato kwa migomo kama hii,” alisema.
Hata hivyo alisema kuwa mgomo huo ni batili kwani hauna baraka za TCCIA mkoa wa Iringa na kuungana na serikali ya mkoa kutaka wahusika wa mgomo huo kusakwa .
Wakizungumzia mgomo huo wafanyabiashara Sara Sanga na Boniface Bukuku walisema wao ni mmoja wa wafanyabishara wa vitu vya urembo pia wanatakiwa kununua mashine hizo.
Alisema Bukuku kuwa kwa mwaka amekadiriwa kulipa kodi ya Sh 574,000 kwa mwaka akiweka na mashine hiyo atalazimika kulipa fedha nyingi zaidi TRA,” alisema.
Akitoa mfano alisema kama mapato yake kwa mwezi ni Sh Milioni 2, atatakiwa kulipa wastani wa Sh200,000 kila mwezi kama kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
“Kwahiyo kwa mwaka nitatakiwa kulipa Sh Milioni 2.4 pamoja na makadiro ya kodi ya Sh 574,000, jumla natakiwa kulipa kiasi kinachokaribia Sh Milioni 3,” alisema.
Alisema kiasi hicho cha kodi ni nje ya kodi ya pango, mishahara ya wafanyakazi na huduma zingine za uendeshaji.
Huku Bi sanga akiadai kuwa TRA mkoa wa Iringa imekuwa ikiwanyanyasa kwa kuwataka kununua mashine hiyo na kuwa wameamua kufunga kutokana na kubanwa kununua mashine hizo bila ya kuwa na elimu ya matumizi yake.
Mbali ya idadi kubwa ya wafanyabiashara kugoma ila baadhi yao walidai kuwa wanalazimishwa kugoma japo wapo tayhari wamenunua mashine hizo na kuiomba serikali kuwawekea ulinzi ili leo waweze kufungua maduka yao .
Meneja wa TRA mkoa wa Iringa Rosalia Mwenda alisema kuwa ofisi yake imeendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kupitia semina mbali mbali na kamwe haijapata kuwanyanyasa wafanyabiashara hao.
Hata hivyo alisema kuwa hakuna atakayewafungia biashara kwa sasa bila ya kuwaandikia barua na kuwataka wafanyabiashara hao kwa wale wasio na elimu ya mashine hizo kufika ofisini kwake .