Na Mwandishi wetu Kenneth John wa matukiodaima.com Dar
Kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarehe 8 Machi,2014, wanahabari nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali na taasisi zisizo za serikali, wameobwa kutangaza na kuelimisha jamii mifano bora inayoonyesha jinsi mwanamke na msichana akipewa fursa na kuwezeshwa hutoa mchango mkubwa sana kwa familia yake na taifa kwa ujumla.
Ombi hilo limetolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kupitia katibu mkuu Anna T. Maembe ambapo amesema kuwa hilo ndilo lengo kuu la kuadhimisha siku hiyo na kuongeza kuwa wanawake ni zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote kwa hiyo wakishirikishwa ipasavyo katika shughuli za maendeleo ni dhahiri mchango wao ni mkubwa sana.
Aidha wizara hiyo imetoa wito kwa mikoa yote kushirikisha wananchi na wadau wote katika kuadhimisha siku hiyo kwa namna watakavyoona inafaa kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu 2014 isemayo “Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia” Na kuongeza kuwa kwa pamoja tunaweza kushiriki kujiletea maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla.
“Ni matumaini yangu kuwa kupitia maadhimisho haya jamii itachochea mabadiliko ya kuachana na mila na desturi zenye madhara na kujikita katika kuboresha ushiriki wa wanawake na wasichana katika kupanga na kutekeleza mipango, mkakati na program za kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kufikia maendeleo endelevu ya nchi yetu”Alisema Maembe.
Pamoja na hayo wizara imebainisha kuwa kila mwaka ifikapo Machi 8 Tanzania huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya wanawake ambapo madhumuni ya maadhimisho hayo ni kutoa fursa ya kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya kimataifa, Kikanda na Kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia .Na huku madhumuni mahususi ya siku hiyo yakiwa ni kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutambua uwezo wa wanawake katika kuchangia kuleta maendeleo endelevu, kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na serikali na wadau katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo yao , familia zao na Taifa kwa ujumla.
Akifafanua kuhusiana na kauli mbiu ya mwaka huu Maembe amesema kuwa ujumbe huo unasisitiza kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, sambamba na muelekeo wa maendeleo kijamii, kitaifa na kimataifa, Na kuongeza kuwa unasisitiza na kuhimiza kuandaa na kutekeleza mipango inayozingatia ushirikishwaji na ushiriki stahiki wa wanawake na wanaume katika kujiletea maendeleo yao.Huku akisema kuwa maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2014 yatafanyika ngazi ya miko.
Sambamba na hayo Maembe amebainisha kuwa maadhimisho hayo pia hutoa fursa maalum kwa Taifa, Mikoa, Wilaya na wadau wengine kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kumwendeleza mwanamke,Lakini pia na kubainisha changamoto zinazowakwamisha kufikia azma ya ukombozi na maendeleo ya wanawake na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.