kulia ni mratibu wa mafunzo hayo Anzawe Chaula akiwa na baadhi ya washiriki waliohudhuria mafunzo hayo akizungumza jambo wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibu katika ukumbi wa Hallfare na kudhaminiwa na kampuni ya Vannedrick ya jijini Dar es salaam kwa kushirikiana asasi isiyo ya kiserikali ya TCDA.
….mwisho…..
Na Denis Mlowe,Iringa
KAMPUNI ya Vannedrick ya jijini Dar es salaam kwa kushirikiana asasi isiyo ya kiserikali ya TCDA wametoa msaada wa kielimu kwa wajasiriamali zaidi ya 200 walioko mkoani Iringa kwa lengo la kuwainua kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Mratibu wa mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibu katika ukumbi wa Hallfare, Anzawe Chaula alisema baada ya kubaini wajasiriamali mkoani Iringa wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa elimu ya biashara ndogondogo na kusababisha wengi wao kushindwa kuendeleza biashara zao wanazozianzisha.
Alisema mafunzo hayo yatawasaidia wajasiriamali kutambua fursa zilizopo katika mkoa wa Iringa na kuwataka kuyafanyia kazi mafunzo hayo waliyopatiwa katika kujikomboa kiuchumi.
Kwa upande wake mgeni rasmi wa mafunzo hayo Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa Iringa Gervas Ndaki akizungumzia kuhusu mafunzo hayo alisema kuwa ni muhimu kwa wajasiriamali kwani ni kati ya fursa za kielimu ambazo zinaweza kuwakwamua na kuondokana na umaskini wakizingatia kwa umakini.
Alisema wajasiriamali hao watanufaika na mafunzo hayo na uwezekano wa kupata mabadiliko makubwa kiuchumi upo kwa sehemu kubwa na hivyo hali ya utegemezi kwa baadhi ya wanawake itapungua.
Ndani alisema pamoja na mafanikio hayo kuna tatizo ambalo kama halitatatuliwa kwa wajasiriamali hao kupatiwa mafunzo kwa ujumla yatakuwa hayana manufaa na kuishia kuwa na kumbukumbu za kwenye daftari na kuwataka waifanyie kazi elimu hiyo waliyopata bure na kuwashukuru wafadhili hao.
“Ni kweli mafunzo haya yamewapa mwelekeo wa maisha wengi hatukuwa na chochote katika ujuzi, lakini mafunzo haya yanahitaji mali ghafi na mitaji lakini kutokana na mafunzo haya utajua ni sehemu gani ya kuanzia na kuweza kujinufaisha katika maisha yako na kuongeza uchumi wa nchi yako na wewe mwenyewe kwa ujumla na itakuwezesha kuendesha miradi inayoibuliwa ”alisema Ndaki.
Ndaki aliwataka wajasiriamali hao kuwa wabunifu katika kuzitumia fursa za elimu na kusikitika kwa kiasi kubwa kwa wajasiriamali wa Iringa kushindwa kujitokeza kwa wingi kama ilivyokuwa malengo ya wafadhili wa mafunzo hayo kukadilia zaidi ya wajasiliamali 1000 kujitokeza.
Aidha alizitaka taasisi za kibenki kupunguza masharti ya mikopo kwa wajasiriamali na kuiomba serikali kutoa hamasa kwa asasi za kifedha za kiserikali na zisizokuwa za kiserikali kuangalia uwezekano wa kuwapa mikopo wajasiriamali wadogo wadogo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuongeza uzalishaji na kukuza pato la Taifa.