Na Mwandishi Wetu
TAMASHA la Pasaka mwaka huu litatimiza miaka 14 tangu kuasisiwa kwake na Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam imekuwa ikijiongezea umaarufu na kukubalika zaidi kutokana na ubunifu wake wa kufanya maadhimisho ya Sikukuu za Pasaka na Krismasi kwa umahiri na mguso wa kiroho kupitia matamasha hayo.
Umaarufu wa matamasha hayo pamoja na mambo mengine, unatokana na ukweli kuwa yamekuwa yakifanyika kwa ubunifu na umakini mkubwa huku kila mwaka yakiongezeka na kubadili waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili wa ndani na nje ya nchi.
Imebainika kuwa tamasha hilo ni kivutio kwa watu mbalimbali kiasi cha kuwafanya kila linapoandaliwa Tamasha la Pasaka na Krismasi, Uwanja wa Taifa uliopo jijini Dar es salaam ambao umekuwa ukitumika kwa kazi hiyo, kufurika watu nao kutoka wakiwa na mioyo iliyotakasika kupitia nyimbo na waimbaji hao.
Hapana shaka kuwa ubunifu huu ndio ulichangia hata Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenela Mukangala, kumteua Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, kuwa Mjumbe wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Matamasha haya yanapambanuliwa na wadau mbalimbali ambao wanayaelezea ubora wake lakini wengi wanasema, yanapata umaarufu na mvuto kwa kuwa washiriki hususan waandalizi na wasanii (waimbaji), wanajiandaa na kujua kinachohitajika kwa jamii, hivyo kukiwasilisha kadiri ya mahitaji ya jamii.
Waimbaji mbalimbali wakiwamo wa kutoka nje ya nchi, wamekuwa wakikonga nyoyo za wananchi kwa kushirikiana vizuri na wazawa.
Sababu ya Kamati za Maandalizi za Matamasha haya kuleta waimbaji kutoka nje ni pamoja na hasa, kuleta ladha tofauti kwa nia ya kupata mahubiri au Neno la Mungu kwa ladha tofauti kutoka kwa waimbaji hao.
Wapo waimbaji wengi wenye uwezo wa kimataifa kutoka nje, lakini hawa ambao wamekuwa wakishiriki katika matamsha haya, ni pamoja na Marehemu Angela Chibalonza (Kenya) ambaye naye aliwahi kutikisa katika Tamasha hili mwaka 2000 lilipoanza, kwa kuimba nyimbo zake.
Baadhi ya nyimbo zake zilizotikisa na kukonga nyoyo ni “Yahwe Uhimidiwe” na “Uliniumba Nikuabudu.”
Wengine walioweka historia nchini ni pamoja na Solly Mahlangu kutoka Afrika Kusini. Mwimbaji huyo aliweza kuvunja rekodi ya waimbaji wote licha ya kuwa hafahamu lugha ya Kiswahili vilivyo, lakini aliweza kuimba nyimbo kadhaa za Kiswahili kama Mwambamwamba ili kwenda sawa na Watanzania aliokonga nyoyo zao kwa kuwapa Neno la Mungu kupitia muziki wa Injili.
Sipho Makhabane, Rebeka Malope nao kwa nyakati tofauti, waliweza kufanya vizuri ukiachilia mbali waimbaji wengine kama Ephraim Sekeleti kutoka Zambia; Ambassadors of Christ (Rwanda), Faraja Ntaboba na Solomoni Mukubwa (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) 24 Elders (Uganda) na Anastazia Mukabwa (Kenya).
Lengo la Msama kuanzisha matamasha haya ni kukusanya mapato kupitia chagizo za viingilio ili kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji maalum wakiwamo wajane, walemavu na kuwasomesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Kwa kiasi kikubwa, Kamati hii imeweza kufanikisha malengo hayo.
Katika matamasha hayo yanayofanyika kila mwaka, wamekuwa wakija waimbaji kutoka nchi tofauti ambapo kwa mwaka huu haijajulikana kwamba ni mwimbaji wepi watakaoshiriki kutoka nje kwa sababu kazi hiyo iko mikononi mwa wananchi ambao wanatakiwa kupiga simu kuchagua mikoa litakapofanyika tamasha hilo, mgeni rasmi na waimbaji.
Uchunguzi wa makala haya kupitia mazungumzo na wadau mbalimbali umebaini kuwa, kila mwaka linapofanyika Tamasha la Pasaka limekuwa likiongezeka ubora ikiwa ni pamoja na kuleta waimbaji wa kimataifa ambako ni wazi kamati hii siku za usoni ikaleta waimbaji wakubwa kutoka nchini za Ulaya na baadaye Marekani.
Kila mwimbaji au kundi la waimbaji linakuwa na vionjo tofauti hivyo tunaamini siku moja kwa kazi nzuri inayofanywa na Msama Promotions, ina uwezo mkubwa wa kuwaleta waimbaji kutoka Marekani kama akina Yolanda Adams, Michael Smith, Martha Carson, Tasha Cobbs na wengine wengi.
Achilia mbali hao, waimbaji wengine kutoka nchi mbalimbali za Afrika ni pamoja na Joyous Celebration, Benjamin Dube, Uche Keke, Sarah K, Paul Kigame na Marion Shako.
“Kamati hii itaendelea kufanya makubwa, hivyo Watanzania na mashabiki wa tamasha hili watarajie kuona mapya tofauti na matamasha mengine yaliyowahi kufanyika ikiwa ni pamoja na kupata Neno la Mungu kupitia waimbaji wapya,” anasema Msama.
Bado ni kitendawili kisichiojulikana kuwa ni mwimbaji gani atakayetoka nje safari hii na kuvunja rekodi ya Solly Mahlangu aliyeimba katika Tamasha Dada la Krismasi lililofanyika Desemba mwaka jana.
Kauli mbiu ya Tamasha hilo ambayo ni ‘Uzalendo Kwanza, Haki huinua Taifa’ itakayochochea na kuimarisha maendeleo ya Tanzania ijayo.