JESHI la polisi mkoani Iringa linamshikilia dereva wa basi aliyejulikana kwa jina la Yusuph Kiponza (35) mkazi wa Mlandege kwa kosa la kusababisha kifo cha abiria wake aliyetambulika kwa jina la Eva Longo (78).
Akizungumza na mtandao huu wa www.matukiodaima.comofisini kwake Kamanda wa polisi mkoani Iringa ACP Ramadhani Mungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea mnamo tarehe 19 machi majira ya saa 12 kamili asubuhi na kusema marehemu alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu baada kugongwa na basi aina ya Scania lenye namba za usajili T. 312 BCE.
Mungi alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva kutokuwa makini kwa abiria wake huyo ambaye alishuka chini wakati akisubiri basi alilokuwa amepanda liondolewe barabarani baada ya kukwama kutokana na utelezi uliokuwepo maeneo ya barabara hiyo ya Usokami – Iringa iliyopo wilaya ya Kilolo.
Kamanda alisema hata hivyo wakati dereva wa gari hilo akiwa katika harakati za kukwepa utelezi huo basi hilo lilimshinda na kwenda kumvaa abiria wake na kumkanyaga miguu yote miwili na hatimaye kuvunjika, hivyo marehemu alikimbizwa Hospitali ya Tosamaganga kwa matibabu zaidi ambapo machi 20 alifariki dunia.
NA DIANA BISANGAO WA MATUKIO DAIMA.COM, IRINGA