Na Kenneth John Matukiodaima.com Dar
Tume ya taifa ya uchaguzi imebaini kuwapo na matumizi ya lugha zisisofaa, kwa baadhi ya vyama vinavyoshiriki katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Chalinze.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi , Jaji Damian Lubuva imebainisha kuwapo na vyama vinavyotumia lugha za chuki na zisizo na staha, na hata kuhamasisha wananchi kuchukua sheria mkononi au kutoa vitisho kwa wapiga kura kwa lengo la kuwazuia wasishiriki katika uchaguzi huo.
Hivyo kutokana na lugha hizo , tume hiyo imelaani vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya vyama vya siasa pamoja na Wagombea.Huku ikiwataka wagombea pamoja na vyama kuzingatia sheria, Kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi yaliyokubaliwa na vyama vyote vya siasa.
Hata hivyo tume imewataka wagombea na vyama vya siasa kukumbuka kuwa, matumizi ya lugha za kejeri zisizo na staha,vitishio na kuzuia wapiga kura kushiriki katika uchaguzi, ni ukiukwaji wa sheria.Na kwa yeyote atakayebainika kukiuka na kuvunja sheria hizo atachukuliwa hatua za kisheria.
Pamoja na hayo tume imevitaka vyama vyote vya siasa, na Wagombea kufanya kampeni za kiungwana na kunadi sera za vyama vyao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote zilizoainishwa katika sheria.
Halikadharika vyama vimetakiwa kutohamasisha wanachama wao kujichukulia sheria mkononi, Na badala yake anayeshukiwa kuvunja sheria akabidhiwe kwenye vyombo vya sheria husika na siyo wao kuamua kutoa adhabu, kwani kwa kufanya hivyo kwa chama chochote ni kinyume na sheria.
Kampeni za uchaguzi huo mdogo katika jimbo la Chalinze , bado zinaendelea kwasasa huku zikitarajiwa kuhitimishwa Aprili 5,2014, na kufuatiwa na uchaguzi utakaofanyiaka Aprili 6,2014.