Quantcast
Channel: Francis Godwin ::Mzee wa matukio daima::
Viewing all articles
Browse latest Browse all 2596

MGOGORO NCHINI MISRI WAACHA MASWALI MANNE KWA JUMUIYA YA KIMATAIFA

$
0
0

Hivi karibuni rais wa muda wa Misri Adli Mansour, amechukua hatua mbalimbali ili kumaliza vurugu na kuondoa mvutano uliopo nchini humo. Lakini licha ya juhudi hizo, hali ya usalama nchini humo bado ni tete. Wachambuzi wanaona kuwa, kuna maswali manne muhimu ambayo bado yanaweka wingu kubwa kwenye hali ya kisiasa ya Misri, na wanaamini kuwa, ili kuiepusha nchi hiyo kuendelea na machafuko, pande zote zinazopingana nchini humo zinatakiwa kuacha vurugu na kuanza mazungumzo ya wazi.
Swali la kwanza linaloulizwa, ni je, suala la rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi, litashughulikiwaje? Tangu rais huyo aondolewe madarakani na jeshi la Misri, hakuna aliyefahamu yuko wapi, hadi jumatano wiki hii baada ya serikali kutoa taarifa zinazomuhusu. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Misri, Badr Abdelatty amewaambia waandishi wa habari kuwa, rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi anashikiliwa katika sehemu ya siri kwa ajili ya usalama wake. Wachambuzi wanasema, katika hali hii ya machafuko, jeshi la Misri linaweza kumzuia rais Morsi asionekane hadharani mapema. Jeshi hilo pia limesema limemwondoa Morsi madarakani kwa kuwa ameshindwa kushughulikia kikamilifu vurugu zilizotokea nchini humo kwa mwaka mzima alipokuwa madarakani. Wachambuzi hao wanasema, njia itakayotumiwa na jeshi na uongozi wa muda wa Misri kushughulikia suala la Morsi itakuwa na athari kubwa kwa mchakato wa mazungumzo ya kisiasa, kwa sababu Morsi hakwenda kinyume na sheria yoyote akiwa rais aliyechaguliwa kwa njia halali.
Swali la pili ambalo watu wengi wanajiuliza, ni je, chama cha Muslim Brotherhood kitachukua hatua gani? Swali hili linatokana na hatua ya serikali ya Misri kutoa hati ya kumkamata kiongozi wa chama hicho Mohamad Badie na viongozi waandamizi kadhaa wa kundi hilo, wakiwatuhumu kwa kuchochea vurugu zilizotokea mjini Cairo. Baada ya rais Morsi kuondolewa madarakani, chama cha Muslim Brotherhood kiliandaa maandamano makubwa kupinga kuundwa kwa serikali ya mpito, na kutoa wito wa kurejeshwa madarakani kwa rais Morsi. Wachambuzi wanasema, chama hicho kinaweza kuchagua kati ya mambo mawili: kuendelea na upinzani au kufikia maafikiano na kutarajia kurudi tena madarakani kwenye uchaguzi bunge na rais katika siku zijazo. Kama chama hicho kikiamua kuendelea na upinzani, kitapambana na jeshi la Misri, hali ambayo haitasaidia kuleta utulivu nchini humo, na pia kwa hali ya baadaye ya kisiasa ya chama hicho.
Jumuiya ya kimataifa pia inajiuliza je, mabadiliko ya kisiasa nchini Misri yatafanyika kwa utulivu? Rais wa mpito wa serikali ya Misri Adli Mansour, amemwapisha kiongozi wa chama cha National Salvation Front, Mohamed El Baradei kuwa makamu wa rais anayeshughulika masuala ya kimataifa, na waziri wa fedha wa zamani bw Hazem al-Beblawi kuwa waziri wa mkuu wa serikali ya mpito. Pia rais huyo ametangaza kuwa uchaguzi mkuu nchini humo utafanyika mapema mwaka kesho. Hatua hii imetoa ishara nzuri ya upatanishi nchini humo, lakini haijulikani kama makundi ya kiislam yanayowakilishwa na chama cha Muslim Brotherhood yatakubaliana na hatua hizo.
Na swali la mwisho: mustakabali wa baadaye wa demokrasia nchini Misri ni upi? Mwezi Februari mwaka 2011, wananchi wa Misri walimwondoa madarakani rais Hosni Mubarak, na sasa, rais aliyechaguliwa kidemokrasia pia ameondolewa madarakani. Wachambuzi wanasema, jambo hilo limerudisha nyuma demokrasia, na pia kuondoa imani ya wananchi wa Misri kwenye suala zima la demokrasia. Mapigano makubwa kati ya makundi mbalimbali ya kidini yanaendelea nchini Misri, na baada ya Morsi kuchukua madaraka, nguvu ya makundi ya kiislam iliongezeka kwa kasi kiasi cha kupuuza mahitaji ya makundi mengine.
Wachambuzi wanasema, njia pekee ya kumaliza machafuko nchini Misri hivi sasa ni kwa pande zote kuacha mapigano haraka na kuonyesha nia yao dhahiri ya kufanya majadiliano ya kisiasa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 2596

Trending Articles