Na Esther Macha,wa matukiodaima.com Mbeya
UTENDAJI wa kazi wa waziri wa uchukuzi ,Dkt.Harrison Mwakyembe umekuwa gumzo katika maeneo mbali mbali nchini huku asilimia kubwa wananchi ikisubiri orodha ya majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini kuwekwa hadharani.
Ninachoweza kusema ni kwamba kauli hizi nimekuwa nikizisikia mara nyingi kutoka kwa viongozi wetu akiwemo, Rais Jakaya Kikwete kuwa angetoa orodha ya vigogo wanaojihusisha na biashara haramu ya mihadarati.
Lakini cha kushangaza kauli hiyo imekuwa kimnya mpaka leo, je waziri Mwakyembe ataweza hili kama kiongozi wake ameshindwa kulifanya hili ?
Ninachoamini ni kwamba kitendo cha kuweka hadharani majina ya watu hao kwa mwakyembe itakuwa ngumu sana kwake hasa ukizingatia kuwa wengine ni watu ambao ni wakubwa wake.
Nionavyo tunachohitaji watanzania ni kuona viongozi wanaosimamia ahadi zao kama Dkt.Mwakyembe na utendaji wa kiongozi huyu utaweza kufanikiwa iwapo hatapewa vitisho vyovyote.
Niseme tu imekuwa kawaida katika nchi yetu ukisema ukweli Fulani kwa jambo ambalo ni maslahi kwa taifa lazima upoteze uhai au kufanyiwa jambo lolote ili kupoteza ushahidi na kukatisha tamaa kwa kile ambacho kinafanywa kwa maslahi ya Taifa.
Suala hili la madawa ya kulevya limekuwa likipigiwa kelele mara nyingi na hata viongozi wengine wamepoteza maisha yao wakati wakipigania suala la dawa za kulevya nchini .
Mimi binafsi ninachoweza kuamini ni kwamba kama kweli nchi hii inahitaji kuwa safi ni vema viongozi wote wakapigania ili kuweza kuondokana na adha hii ambayo imesababisha vijana wengi kuharibikiwa katika maisha kutokana na madawa hayo.
Pia kama viongozi wengine ni muhimu wakaiga na kumpa ushirikiano wa kutosha kufanikisha zoezi hili kwani peke yake hawezi hivyo apewe ushirikiano ili aweze kufanikisha kazi hii.
Ushauri wangu kwa serikali kama kweli inahitaji kujisafisha kuhusiana dawa za kulevya haina budi kuwa bega kwa bega na Waziri Mwakyembe ili kuweza kuwafichua wauza dawa ,lakini endapo suala hili ataachiwa hakuna chochote ambacho kitafanyika zaidi ya kuishia kutamka .
Kitu ambacho kinafanya juhudi za dawa za kulevya kukomeshwa ni kutokana viongozi wetu wa serikali kutopenda mtu ambaye anasema ukweli halisi wa jambo ,kama kweli ukweli ungekuwa unakubalika sidhani kama tungefika hapa tulipo hivi sasa.
Nionavyo katika hili ni kwamba hata kama ikitokea wametajwa wahusika ninachoweza kusema ni kwamba watakaoweza kutajwa ni vidagaa tu lakini samaki wenyewe wakubwa halisi kuachwa .
Waziri Mwakyembe juzi alifanya ziara hiyo JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku chache baada ya kutokea kashfa ya kupitishwa kwa dawa za kulevya na baadhi ya Watanzania wakiwamo wasanii kukamatwa sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumzia watendaji wa JNIA kuhusiana na dawa za kulevya, alisema: “Mfanyakazi yeyote atakayebainika kuhusika kuwasaidia wasafirisha unga atafukuzwa kazi na ambaye atafanya juhudi ya kuwakamata wasafirishaji hao atapewa zawadi.”
Juhudi za Mwakyembe ziungwe mkono na watu wote ili kunusuru janga hili ambalo limekuwa sugu miaka mingi licha ya viongozi wengi kujitahidi kulivalia njuga lakini bado limekuwa ni tatizo kubwa kadri siku zinavyozidi kwenda.