1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kutokana na Taarifa zilizowasilishwa katika Bunge lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa Mwaka 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2014/2015.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote na kwa masikitiko makubwa naomba nichukue fursa hii kutoa salamu za pole kwako na kwa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na wabunge wawili, Mheshimiwa William Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga, aliyefariki tarehe 01 Januari, 2014 na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze, ambaye alifariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, niwape pole Wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kifo cha Mheshimiwa John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, kilichotokea tarehe 25 Machi 2014, na kwa Wananchi wa Wilaya ya Urambo kwa kifo cha Mheshimiwa Anna Magowa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, kilichotokea tarehe 24 Septemba 2013. Vilevile, natoa pole kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo kwa kifo cha Mheshimiwa Moshi Mussa Chang’a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, aliyefariki tarehe 21 Aprili 2014. Naomba pia niwape pole Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote waliofiwa na ndugu na jamaa zao kutokana na majanga na matukio mbalimbali tangu nilipowasilisha Bajeti yangu ya mwaka 2013/2014.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina! Nichukue fursa hii pia kuwapa pole Wahanga wote wa majanga mbalimbali yakiwemo mafuriko na ajali za barabarani, na niwashukuru kwa dhati wote waliotoa misaada ya hali na mali wakati wa ajali na maafa hayo.
3. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014, Bunge lako Tukufu limepata Wabunge wapya watatu ambao ni Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze. Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha Wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawaomba watumie fursa waliyoipata kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
4. Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili tangu tuanze utaratibu wa Mzunguko mpya wa Bajeti ambao unatuwezesha kukamilisha Mjadala wa Bajeti ya Serikali ifikapo tarehe 30 Juni ya kila mwaka. Taarifa za awali zinabaini kwamba utaratibu huu umeanza kuonesha mafanikio ya haraka katika utekelezaji wa kazi zilizopangwa. Bajeti hii imeendelea kutayarishwakwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN). Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kipaumbele iliyoainishwa kwenye mipango hiyo ya Kitaifa ili kuleta maendeleo endelevu na ya haraka yatakayowanufaisha Wananchi wa Tanzania.
5. Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi waliyoifanya ni kubwa na ambayo imetuwezesha kukamilisha maandalizi ya Bajeti ninayoiwasilisha leo. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.
HALI YA SIASA
6. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya siasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu yao. Nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mpito ambapo tunaandika Katiba Mpya itakayoweka mustakabali wa mwelekeo wa Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Nawasihi Wanasiasa na Wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa maandalizi ya Katiba hiyo ambayo baadaye wananchi wote wataipigia kura ya maoni. Nawaomba tushindane kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu katika kuandaa Katiba hii ambayo itatuongoza sasa na vizazi vijavyo.
7. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi Nchini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeratibu shughuli za Vyama vya Siasa kwa kuhakikisha kunakuwepo na fursa sawa katika shughuli za siasa Nchini. Hadi Aprili 2014, idadi ya Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa kudumu imefikia 21 baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kupata usajili wa kudumu mwezi Juni, 2013. Aidha, Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-TANZANIA), Chama cha Wananchi na Demokrasia (CHAWADE) na Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) vimepata usajili wa muda. Nirejee wito wangu kwa Viongozi na Wanachama wa vyama vyote vya siasa kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana na kutohamasisha siasa za chuki na vurugu ambazo zinaweza kutugawa na kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa Taifa letu tulioujenga kwa miaka mingi.
ULINZI NA USALAMA
8. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kudumisha amani na utulivu kama tunu ya Taifa iliyojengwa na kuimarishwa tangu tulipopata uhuru. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Jeshi na Mkakati wa Kupunguza Uhalifu ambavyo vimeongeza ushirikiano na wananchi. Jeshi hilo limeongeza Vikundi 1,778 vya Ulinzi Shirikishi na kufikia vikundi 6,798 kwa mwaka 2013 kwa Nchi nzima. Vikundi hivyo vimechangia kupunguza vitendo vya uhalifu Nchini kutoka Asilimia 4.3 mwaka 2012 hadi Asilimia 2.8 mwaka 2013 na hivyo kuchangia kupungua kwa makosa makubwa na madogo ya jinai kutoka makosa 566,702 mwaka 2012 hadi makosa 560,451 mwaka 2013.
9. Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, hivi karibuni kumetokea wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake. Katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2014, wanawake wanane (8) wameuawa kikatili katika Kata za Mugango, Etaro, Nyakatende na Nyegina Wilayani Butiama. Uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, mauaji hayo yamefanyika mchana na kwa mtindo unaofanana wa kunyongwa na kanga au kamba na miili yao kufukiwa kwenye mashimo mafupi au kufichwa vichakani. Mara zote walengwa ni wanawake wanapokuwa kwenye shughuli zao za kilimo.
10. Mheshimiwa Spika, Serikali inalaani vitendo hivyo visivyokubalika katika jamii na itawachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote. Serikali imechukua hatua kadhaa za kudhibiti vitendo hivyo vya mauaji ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa 26 na kati yao 13 wamefikishwa mahakamani. Vilevile, Jeshi la Polisi limeunda kikosi kazi kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo na kufanya mikutano ya kuhamasisha jamii kuhusu kuanzisha na kuimarisha vikundi vya Polisi Jamii. Nitoe wito kwa wananchi wema, wenye upendo na Nchi yetu kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye vyombo vya usalama ili Sheria ichukue mkondo wake.
Ajali za Barabarani
11. Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani zimeendelea kuwa tishio kwa maisha ya watu na mali zao. Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa katika mwaka 2013, kulitokea ajali za barabarani 24,480 zilizosababisha vifo vya watu 4,091 na majeruhi 21,536 ikilinganishwa na ajali 23,604 zilizosababisha vifo vya watu 4,062 na majeruhi 20,037 mwaka 2012. Kwa upande wa pikipiki pekee, mwaka 2012 zilitokea jumla ya ajali 5,763 na kusababisha vifo 930 na majeruhi 5,532. Mwaka 2013, zilitokea ajali 6,831 na kusababisha vifo 1,098 na majeruhi 6,578. Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2014 zimetokea ajali 1,449 na kusababisha vifo 218 na majeruhi 1,304. Ajali hizi ni nyingi na zinasababisha vifo vingi na majeruhi ambao wengi wao ni nguvukazi ya Taifa. Ni vyema ikumbukwe kwamba, Serikali iliruhusu matumizi ya pikipiki kwa nia njema ya kupunguza matatizo ya usafiri hususan maeneo ya Vijijini. Hata hivyo, fursa hiyo imeambatana na changamoto ya ajali nyingi barabarani. Hivyo ni wajibu wa madereva wote kuzingatia sheria za barabarani na kukidhi vigezo vyote vya kuwa na vibali halali vya kufanya biashara hizo pamoja na leseni za udereva. SUMATRA, Jeshi la Polisi, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Mamlaka nyingine zinazohusika zinatakiwa kukaa pamoja ili kuweka mkakati wa kukabiliana na ajali hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Kanuni za Leseni za Usafirishaji wa Pikipiki na Bajaji za mwaka 2010zinatekelezwa ipasavyo.
12. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutimiza majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi yetu na raia wake. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imewezesha Wanajeshi wetu kupata mafunzo mbalimbali katika vyuo vya ndani na nje ya Nchi pamoja na kushiriki katika mazoezi ya ushirikiano kikanda. Aidha, Jeshi limeshiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa huko Darfur (Sudan), Lebanon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini. Nafurahi kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa Jeshi limefanya kazi kubwa, nzuri na kwa weledi mkubwa, nidhamu na kujituma hivyo kuendelea kuipatia heshima kubwa Nchi yetu. Katika jitihada za kuwapatia Askari mazingira mazuri ya kuishi, Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za Askari ambapo ujenzi wa majengo 191 kati ya 6,064 unaendelea katika vikosi mbalimbali vya Jeshi Nchini.
13. Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014 ni wa tatu tangu Serikali iliporejesha utaratibu wa kuwachukua Vijana wanaohitimu kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria. Hadi kufikia mwezi Desemba 2013, jumla ya Vijana 15,167 wamehitimu mafunzo ya JKT wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili Tukufu. Mafunzo hayo yamewapatia vijana hao fursa ya kujifunza juu ya Ulinzi, Usalama na Ukakamavu, Uzalishaji mali, Uzalendo na Umoja wa Kitaifa. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itachukua vijana zaidi kujiunga na JKT kwa Mujibu wa Sheria.
SHUGHULI ZA UCHAGUZI, BUNGE, MUUNGANO, MABADILIKO YA KATIBA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
14. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisimamia na kuendesha chaguzi ndogo za Wabunge katika Majimbo matatu na Udiwani katika Kata 53 nchini. Chaguzi hizo zimefanyika kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vifo na baadhi ya Waheshimiwa Madiwani kukosa sifa za kuendelea na nyadhifa hizo. Katika Uchaguzi wa Ubunge uliofanyika katika Jimbo la Chambani - Zanzibar, CUF ilishinda kwa kupata Asilimia 84 ya kura zote. CCM ilipata kura Asilimia 12.4, ADC ilipata kura Asilimia 3.5 na CHADEMA ilipata Asilimia 0.4 ya kura zote. Katika Jimbo la Kalenga – Iringa, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia 79.3 ya kura, CHADEMA ilipata kura Asilimia 20.2 na CHAUSTA ilipata kura Asilimia 0.5. Katika Jimbo la Chalinze – Pwani, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia 86.61, CHADEMA ilipata kura Asilimia 10.58, CUF ilipata kura Asilimia 1.98, AFP ilipata kura Asilimia 0.59 na NRA ilipata Asilimia 0.25 ya kura zote. Aidha, katika Chaguzi za Madiwani zilizofanyika katika Kata 53, CCM ilishinda viti 40, CHADEMA viti 12 na NCCR – Mageuzi kiti kimoja (1).
15. Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na maandalizi ya kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Katika awamu hii ya uboreshaji wa Daftari, Mfumo wa Biometric Voter Registration utatumika tofauti na Mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji. Mfumo huu wa kisasa unawezesha uandikishaji na uchukuaji wa alama za vidole kwa haraka zaidi na hatimaye mwananchi kupatiwa kitambulisho cha kupiga kura kwa muda mfupi. Hii itasaidia sana kuokoa muda na kupata takwimu sahihi za wapiga kura watakaoshiriki kwenye chaguzi.
16. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa kuhamasisha Wanachama na Watanzania wote wenye sifa kujiandikisha kwenye Daftari hilo na kupata kitambulisho halali cha mpiga kura pale zoezi hilo litakapoanza rasmi. Aidha, ninatoa wito kwa Wananchi wote wenye sifa kujitokeza kujiandikisha. Ni imani yangu kwamba tukitumia fursa hii kikamilifu tutaondoa malalamiko ya majina ya baadhi ya wapiga kura kutokuwepo kwenye orodha wakati wa chaguzi. Ni muhimu tukumbuke kwamba ni wananchi wenye sifa tu ndiyo watakaoandikishwa. Katika mwaka 2014/2015, Tume itakamilisha zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kusimamia Kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Mpya, na kuendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa Wananchi.
Bunge
17. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai, 2013 hadi Aprili 2014, Ofisi ya Bunge imeendesha Mikutano Mitatu ya Bunge na Mikutano mitatu ya Kamati za Bunge. Maswali ya Msingi 410 pamoja na maswali 73 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa. Aidha, Miswada minane (8) ya Sheria ilipitishwa na Bunge. Pia, Bunge limekamilisha ukarabati wa Ukumbi wa Bunge na Miundombinu yake kuwezesha Mkutano wa Bunge la Katiba kufanyika na ujenzi wa Ofisi za Wabunge Majimboni umeendelea kufanyika. Vilevile, Ofisi ya Bunge imewajengea uwezo Wabunge na Watumishi wake kupitia semina mbalimbali katika masuala ya Utawala Bora. Katika mwaka 2014/2015, Ofisi ya Bunge itaendelea kuratibu Mikutano ya Bunge, Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na kuimarisha miundombinu na majengo ya Bunge.
Muungano
18. Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Aprili 2014, tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo kipindi kifupi. Tumeweza kufika hapa tulipo kutokana na misingi imara ya Muungano iliyowekwa na Waasisi wetu na kuendelezwa na Viongozi walioongoza Taifa letu katika awamu zilizofuatia. Tunajivunia kwamba Muungano wa Tanzania umejengeka kwenye historia ya muda mrefu ya ushirikiano wa watu wa pande hizi mbili. Jamii hizi zina uhusiano wa damu, kifikra na mapambano ya pamoja dhidi ya wakoloni waliotawala kwa vipindi tofauti. Walichofanya waasisi wetu mwaka 1964 ni kurasimisha ushirikiano wetu wa muda mrefu. Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano. Aidha, ninawashukuru kwa dhati Viongozi wote walioongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar tangu kuasisiwa kwa Muungano. Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Uongozi wao ambao umezifanya pande mbili za Muungano kuwa karibu zaidi.
19. Mheshimiwa Spika, tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano tukiwa na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Takwimu hizo zinaweka jambo moja wazi kwa Muungano wetu; kwamba zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wote wamezaliwa baada ya Muungano. Hivyo, tuliozaliwa kabla ya Muungano ni chini ya asilimia kumi. Kwa mujibu wa takwimu hizo, Tanzania nzima ina watu 44,926,923. Kati yao, watu 40,640,425, sawa na Asilimia 90.6 ni wa umri wa siku moja hadi miaka 50. Kwa upande wa Tanzania Bara, idadi ya watu ilikuwa 43,625,354, kati ya hao, watu 39,456,065 sawa na asilimia 90.5 wamezaliwa baada ya Muungano. Kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na watu 1,303,569, ambapo watu 1,184,360 sawa na asilimia 90.9 wamezaliwa baada ya Muungano. Takwimu hizo zina maana kwamba, asilimia 90.6 ya watu wote wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.
20. Mheshimiwa Spika, tuna kila sababu ya kuadhimisha Miaka hii 50 ya Muungano kwa furaha. Katika maadhimisho ya mwaka huu, tuliandaa maonesho maalum, makongamano na shughuli nyingine ambazo zilisaidia wananchi kuelimishwa kuhusu masuala ya Muungano. Aidha, kimeandaliwa kitabu maalum kinachoelezea historia, utekelezaji wa mambo ya Muungano, mafanikio, changamoto, fursa na matarajio ya Muungano kwa miaka ijayo. Kitabu hicho kitatumika kama rejea kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.
21. Mheshimiwa Spika,tutaendelea kuulinda Muungano wetu kwa nguvu zote tukiwa na uelewa kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita Watanzania wameishi kwa amani na kufanya kazi zao za kujiletea maendeleo wakiwa upande wowote wa Muungano. Tunatambua changamoto zilizopo na tumeweka utaratibu mzuri wa vikao ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo. Vikao hivyo vitaendelea kufanyika katika ngazi ya wataalam, Watendaji Wakuu na Viongozi wa Kitaifa. Ni imani yangu kwamba, Muungano huu utaendelea kudumu na watu watapata maendeleo makubwa kwani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina fursa nyingi zinazoweza kutumika kwa manufaa ya wote. Sote tukumbuke kuwa, UTANZANIA WETU NI MUUNGANO WETU, TUULINDE, TUUIMARISHE NA KUUDUMISHA!
Mabadiliko ya Katiba
22. Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Desemba 2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikamilisha Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuikabidhi kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Napenda kuishukuru Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rasimu hiyo imeliwezesha Bunge Maalum la Katiba kuanza mjadala. Nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania wote kwa kutoa maoni yaliyowezesha Tume kuandaa Rasimu hiyo ya Katiba.
23. Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la Katiba linaundwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe 201 walioteuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa kupata fursa hii ya kuwawakilisha Watanzania katika kuandaa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni dhahiri kuwa dhamana hii ni kubwa sana!
24. Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la Katiba lilianza kazi rasmi tarehe 18 Februari, 2014 kwa kumchagua Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kulisimamia Bunge Maalum hadi kuwezesha kupatikana kwa Kanuni za kuliongoza Bunge hilo. Aidha, niwapongeze Mheshimiwa Samwel John Sitta kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba. Nampongeza Katibu wa Bunge la Katiba Bwana Yahaya Hamadi Khamis na Naibu wake Dkt. Thomas Kashililah pamoja na Wajumbe wote waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati 12 za Bunge Maalum. Baada ya kukutana kwa muda wa siku 67, Bunge Maalum limeahirisha Mkutano wake tarehe 25 Aprili, 2014 ili kupisha majadiliano ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015. Ni matumaini yangu kwamba, Bunge Maalum la Katiba litakaporejea litakamilisha kazi hiyo kwa umakini na kupata Rasimu ambayo hatimaye itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni.
25. Mheshimiwa Spika,katika hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2013/2014 nilielezea dhamira ya Serikali ya kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa Wananchi wake. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imekamilisha usajili na utambuzi wa watu kwa upande wa Zanzibar, Watumishi wa Umma na vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa vituo vya kuingiza na kuhakiki taarifa, kituo cha kutengeneza Vitambulisho na kuhifadhi kumbukumbu pamoja na kituo cha uokozi na majanga ya taarifa na takwimu. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na zoezi la Utambuzi na Usajili wa Watanzania katika Mikoa mingine ili kwa pamoja tuweze kunufaika na Vitambulisho vya Taifa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kiusalama.
Sensa ya Watu na Makazi
26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea kutoa machapisho mbalimbali ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Machapisho hayo yanajumuisha Taarifa ya Mgawanyo wa Watu kwa Maeneo ya Utawala; Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia na Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi. Taarifa hizo zimebaini kuwa, katika miaka kumi iliyopita kumetokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika kimeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi asilimia 78 mwaka 2012. Aidha, uandikishaji halisi katika shule za msingi umeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi 77 mwaka 2012. Idadi ya watu wanaoishi kwenye nyumba zenye kuta imara ni asilimia 74 na asilimia 65.4 wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa bati. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo,
hali ya utegemezi nchini ni kubwa kutokana na ukweli kuwa kati ya Watanzania Milioni 44.9, Asilimia 50.1 ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Aidha, takwimu zimebainisha kuwa Asilimia 7.7 ya Watanzania ni watoto yatima. Kutokana na hali hiyo, ni jukumu letu kama Taifa kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo katika sekta za huduma za jamii ili hatimaye kila mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie ipasavyo katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi yetu.
MASUALA YA UCHUMI
Hali ya Uchumi
27. Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa katika mwaka 2013 lilikua kwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 mwaka 2012. Ongezeko hilo limetokana na ukuaji mzuri wa shughuli za huduma za mawasiliano, viwanda, ujenzi na huduma za fedha. Kutokana na ongezeko hilo, wastani wa Pato la Mtanzania limeongezeka kutoka Shilingi 1,025,038 mwaka 2012 hadi Shilingi 1,186,424 mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 15.7. Mfumuko wa Bei umepungua kutoka Asilimia 9.8 Machi 2013 hadi Asilimia 6.1 Machi 2014. Kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya kupanda bei za bidhaa na vyakula hasa mahindi, mchele na aina nyingine ya nafaka.
28. Mheshimiwa Spika, pamoja na uchumi wetu kukua kwa kasi ya asilimia 7.0 kwa mwaka 2013 na Pato la Mtanzania kuongezeka, kiwango hicho siyo kikubwa sana kuwezesha umaskini wa wananchi kupungua kwa kasi. Utafiti wa kitaalam unaonesha kwamba, ili umaskini upungue kwa kasi kubwa, uchumi unatakiwa kukua kwa zaidi ya Asilimia 8 kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo. Ukuaji huo pia unatakiwa kulenga Sekta ambazo zinagusa maisha ya watu wengi, hususan kilimo, mifugo na uvuvi. Mwelekeo wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta za kipaumbele kukua kwa kushirikisha Sekta Binafsi.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
29. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016 ambao unatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali ilitekeleza Mpango huo kupitia Kauli mbiu ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Msingi wa kauli mbiu hii ni kuainisha maeneo machache ya kimkakati na kuyatengea rasilimali za kutosha, kusimamia na kufuatilia utekelezaji kwa karibu zaidi. Chombo maalum cha Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi ya kimkakati chini ya Ofisi ya Rais kinachojulikana kama President’s Delivery Bureau– (PDB) kimeanzishwa na Watendaji Wakuu wameteuliwa. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, matunda ya utekelezaji wa Mfumo huo yameanza kuonekana katika maeneo makuu sita ya kipaumbele kitaifa ambayo ni Nishati ya Umeme, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa Mapato. Utekelezaji wa miradi hiyo na mafanikio yaliyoanza kupatikana yatatolewa maelezo na Mawaziri katika Sekta husika.
30. Mheshimiwa Spika, njia ya uhakika ya kuliwezesha Taifa kuwa na uchumi imara na wa kisasa utakaohimili ushindani katika masoko ya Kikanda na Kimataifa ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji. Katika kufikia azma hiyo, tarehe 31 Januari, 2014 nilizindua rasmi Taarifa ya Tathmini ya Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji Tanzania. Mapendekezo ya Taarifa hiyo yatatumika kuihuisha Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 pamoja na Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 1997. Aidha, ili kuwawezesha Wawekezaji na Wafanyabiashara kupata huduma na taarifa zote muhimu kama vile Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali kuhusu biashara na uwekezaji kwa njia ya mtandao, Serikali imezindua upya Tovuti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Kupitia Tovuti hii, Wawekezaji popote duniani wanaweza kupata taarifa kuhusu usajili wa Kampuni na viwango vya kodi kwa njia ya mtandao.
Dhamira ya Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza gharama za kufanya biashara nchini ili kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka nchi nyingine zilizotekeleza maboresho ya mifumo yao ya udhibiti wa biashara.
31. Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi inaendelea kupewa nafasi kubwa katika kukuza uchumi Nchini. Takwimu zinaonesha kwamba, Miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania imeongezeka kutoka 869 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 31.5 mwaka 2012 hadi miradi 885 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 141.2 mwaka 2013.
Napenda pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Nchi nyingi duniani zinaendelea kuiamini Tanzania kama Kituo maarufu cha uwekezaji Duniani. Mwezi Novemba, 2011 nilizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza unaojulikana kama Partnership in Prosperity. Mpango huo umelenga kuongeza uwekezaji kutoka Sekta Binafsi ya Uingereza kwenye mafuta na gesi, kilimo na Nishati jadidifu. Lengo ni kuongeza uwekezaji kutoka Nchi hiyo kwa zaidi ya maradufu ya kiwango cha sasa. Aidha, tumekubaliana kushirikiana kuimarisha mazingira ya biashara ili kurahisisha uwekezaji katika sekta hizo.
32. Mheshimiwa Spika, baadhi ya Kampuni za Uingereza tayari zimeanza kutekeleza makubaliano hayo kwenye Sekta ya kilimo. Kampuni ya Unilever kwa mfano, itawekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 275 kwenye kilimo cha chai kwa kushirikiana na wakulima wadogo. Tayari Kampuni hiyo imeanza kupanua Kiwanda cha Chai Kibwele, Mufindi na kufungua zaidi ya Hekta 300 za mashamba ya chai katika Wilaya ya Mufindi. Aidha, Kampuni hiyo imeingiza nchini vipando 250,000 vya miche bora ya chai. Pia, Kampuni inaandaa zaidi ya miche milioni 2 kwa ajili ya kuwagawia wakulima wadogo Wilayani Njombe ili waongeze uzalishaji wa chai Nchini.
33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014,Kituo cha Uwekezaji kimeshirikiana na Uongozi wa Mikoa mbalimbali Nchini kuratibu maandalizi ya Makongamano ya Uwekezaji yenye lengo la kuhamasisha, kukuza na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo. Jumla ya Mikoa 11 imeshiriki kikamilifu kuandaa na kufanikisha Makongamano ya Uwekezaji katika maeneo yao. Mikoa hiyo ni Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Manyara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Makongamano hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo, pamoja na kuihamasisha Mikoa na Halmashauri za Wilaya ndani ya Mikoa hiyo kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Aidha, Wawekezaji wengi walioshiriki kwenye Makongamano hayo wameonesha nia na utayari wa kuwekeza kwenye Mikoa husika. Jitihada hizi zitaendelezwa katika kipindi kijacho.
34.Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yangu ya Bajeti mwaka 2013/2014, nilieleza kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote. Mkutano huo ulifanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 1 Julai 2013, Jijini Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huo ulitoa fursa ya kipekee kwa Viongozi wa Serikali kujadiliana na kupata maoni ya makundi mbalimbali ya Wananchi kuhusu mbinu za kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Serikali imedhamiria kufanya Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote kila mwaka kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa kwa kuzingatia fursa kubwa za maendeleo shirikishi zilizopo kwenye maeneo husika.
35.Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Biashara lilifanya Mkutano wake wa Saba tarehe 16 Desemba 2013 chini ya Kauli Mbiu ya “Ukuaji Shirikishi wa Uchumi”. Maazimio ya Mkutano huo ni pamoja na kuunda Kamati Tatu ambazo zitashughulikia Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mazingira Wezeshi ya Biashara na Matumizi Endelevu ya Maliasili za nchi. Kamati ya Mazingira Wezeshi ya Biashara imeanza kuishauri Serikali kuhusu mikakati ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania. Kazi hiyo imefanyika kwa utaratibu wa Maabara chini ya Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Utaratibu huo ulianzisha maeneo sita muhimu ambayo yakishughulikiwa yataboresha mazingira ya biashara nchini. Maeneo hayo ni kuboresha Kanuni na Taasisi zinazosimamia biashara; upatikanaji wa ardhi na haki za umiliki wake na kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupunguza wingi wa kodi na tozo mbalimbali. Maeneo mengine ni kuzuia na kupambana na rushwa; kuboresha Sheria za Kazi na kuimarisha mafunzo na stadi za kazi pamoja na kusimamia utekelezaji wa mikataba na utawala wa sheria. Katika mwaka 2014/2015, Baraza la Taifa la Biashara litaendelea kuratibu utekelezaji wa maazimio hayo ya Mkutano wa Saba sanjari na kusimamia mikutano ya Mabaraza ya Wilaya na Mikoa.
36. Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya kubuni na kutekeleza Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ni kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao badala ya kubaki kuwa watazamaji.Kwa kutambua umuhimu wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, katika Mwaka 2013/2014Serikali imeanzisha Taasisi ya Ujasiriamali na Ushindani wa Kibiashara (Tanzania Entrepreneurship Competitiveness Centre). Taasisi hiyo itatekeleza jukumu la kutoa miongozo ya uandaaji wa mitaala ya ujasiriamali katika ngazi tofauti na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa bora zitakazohimili ushindani. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kuongeza ufanisi wake. Hadi kufikia mwezi Februari 2013, Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi ulikuwa umepokea Shilingi Bilioni 2.1 zilizotumika kudhamini mikopo ya wajasiriamali kupitia Benki ya CRDB kwa makubaliano ya kukopesha mara tatu ya dhamana ya Serikali. Kutokana na makubaliano hayo, hadi kufikia mwezi Desemba 2013, mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shillingi Bilioni 9.5 ilikuwa imetolewa kwa Wajasiriamali 9,790 waliojiunga kwenye Vikundi 283 na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) 51 katika Mikoa 12 na Wilaya 27.
37. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, hadi kufikia Desemba 2013, ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 36.39 kwa Wajasiriamali 62,720. Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulikuwa umetoa mikopo kwa Vijana yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.22 kupitia SACCOS 244; na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.44 kwa Wanawake 500,000 Nchini. Vilevile, Mradi wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF) ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 57.1 kupitia Asasi 375 za Kifedha ambapo Wajasiriamali 95,034 walinufaika.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF
38.Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zilizo katika Mazingira Hatarishi Tanzania Bara na Zanzibar. Katika kutekeleza Mpango huo, utaratibu wa uhawilishaji fedha kwa kaya maskini ulifanyika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 22 ambapo kaya 138,032 katika Vijiji na Shehia 1,179 zilitambuliwa na kuandikishwa katika Mfumo wa Masijala wenye walengwa 464,552. Hadi sasa, Shilingi Bilioni 5.5 zimehawilishwa katika kaya hizo. Lengo ni kuziwezesha kaya hizo kupata chakula na kujiongezea fursa ya kipato.
39. Mheshimiwa Spika,Serikali pia imejenga uwezo kwa Viongozi na Wataalam kutoka maeneo ya utekelezaji wa Mpango huo. Uwezo umejengwa kwa kutoa mafunzo katika masuala ya utambuzi, uandikishaji na ukusanyaji taarifa za kaya maskini. Aidha, mafunzo ya usanifu wa miradi ya ujenzi yalitolewa kwa wataalam kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia, Wajumbe 17 wa Baraza la Wawakilishi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka Zanzibar walitembelea Vijiji vya Pongwe-Kiona na Malivundo (Bagamoyo) na Gwata (Kibaha) ili kujifunza kuhusu utekelezaji bora wa Mpango huo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kufanya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini kufikia maeneo yote 161 ya utekelezaji wa Mpango Tanzania Bara na Zanzibar. Lengo ni kutambua na kuandikisha Kaya 920,000 kutoka Vijiji, Mitaa na Shehia 9,000.
UZALISHAJI MALI
Uzalishaji wa Mazao
40. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa chakula ni ya kuridhisha katika maeneo mengi nchini kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa 2012/2013. Uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu huo ulikuwa Tani Milioni 14.38 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya Tani 12.15 kwa mwaka 2013/2014 ikiwa ni ziada ya Tani Milioni 2.3 za chakula. Ongezeko hilo limefanya Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 118 na hivyo, kufanya wastani wa bei za mazao ya chakula katika masoko Nchini kuwa za chini katika kipindi chote cha mwaka 2013/2014.
41. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na juhudi za kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kulingana na Mipango inayotekelezwa chini ya Kaulimbiu ya KILIMO KWANZA, na Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imesambaza jumla ya vocha za ruzuku 2,796,300 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 83 kwa ajili ya mbolea na mbegu bora za mpunga na mahindi kwa Kaya 932,100. Pia, Serikali ilitoa ruzuku ya dawa za korosho kiasi cha lita 158,845 na Tani 620 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5. Vilevile, ruzuku ilitolewa kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za pamba Tani 4,000 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.8, miche ya kahawa 350,000 yenye thamani ya Shilingi Milioni 100 na miche ya chai 1,850,000 yenye thamani ya Shilingi Milioni300.
42. Mheshimiwa Spika, ongezeko la tija katika uzalishaji wa mazao unategemea sana huduma bora za ugani kwa wakulima. Serikali katika mwaka 2013/2014, ilitoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani 1,452 ili kufanikisha kufikiwa kwa malengo ya kuwa na Afisa Ugani wa Kilimo mmoja kwa kila kijiji. Vilevile, Serikali imeongeza Mashamba Darasa kutoka 16,330 yenye wakulima 344,986 mwaka 2012/13 hadi 16,543 yenye wakulima 345,106 mwaka 2013/2014 ili kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima.
43. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikisha Washirika wa Maendeleo kuchangia Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT). Miongoni mwa malengo ya Programu hiyo ni kuwaunganisha wakulima wadogo na mnyororo wa thamani wa kibiashara wa Makampuni makubwa ya ndani na nje ya nchi. Ili kufikia lengo hilo, Serikali imeanzisha Mfuko Chochezi wa Uendelezaji wa Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT Catalytic Trust Fund). Mfuko huo utatoa mitaji itakayogharamia hatua za awali za miradi inayotoa tija ya haraka ambayo imebainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Uwekezaji. Vilevile, Mfuko huo utahamasisha biashara inayolenga kumuinua Mkulima mdogo kwa kumuunganisha na mnyororo wa thamani na kampuni kubwa kupitia madirisha makuu mawili. Dirisha la kwanza ni Matching Grant Fund linalolenga kuwezesha kampuni kubwa zilizoanzisha biashara ya Kilimo Nchini, kuimarisha minyororo ya thamani inayowahusisha wakulima wadogo zaidi au kuanzisha kilimo cha Mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima wadogo. Dirisha la pili ni Social Venture Capital Fund, linalolenga kuziwezesha biashara changa na za kati kwenye Sekta ya Kilimo au kuwezesha Kilimo cha mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima wadogo. Tayari Bodi ya Mfuko imeteuliwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko ameajiriwa.
44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, inategemea kuvutia uwekezaji na kuanzisha Kilimo cha mashamba makubwa 25 ya Kilimo cha kibiashara kwa mazao ya mpunga na miwa kwa utaratibu wa kuwaunganisha wakulima wakubwa na wadogo wanaozunguka mashamba hayo. Aidha, itaanzisha, itaboresha na kuendesha kitaalamu maghala 275 ya kuhifadhi mahindi kwa kuwaunganisha wakulima katika umoja wa kibiashara kwa ajili ya kupata masoko ya pamoja.
Umwagiliaji
45. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendeleza Kilimo cha umwagiliaji Nchini, Sheria ya Umwagiliaji Namba 5 ya mwaka 2013 imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo itaiwezesha Serikali kuanzisha Tume ya Umwagiliaji ambayo ni chombo cha kitaifa chenye dhamana ya kusimamia, kuendeleza na kudhibiti shughuli za Umwagiliaji Nchini. Sheria hiyo pia itaanzisha Mfuko wa Taifa wa Umwagiliaji utakaosaidia kutekeleza mipango ya umwagiliaji kwa kulipia gharama za umwagiliaji zinazofanywa na mkulima mmoja mmoja na wawekezaji kupitia mikopo na dhamana. Serikali pia iliendelea na ujenzi na ukabarati wa skimu 24 za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 15 Nchini. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendeleza Skimu za Umwagiliaji 39 kwa ajili ya Kilimo cha mpunga.
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kupitia Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini imekarabati kilometa 352 za barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe katika Halmashauri za Iringa Vijijini, Njombe Vijijini, Singida Vijijini, Mbarali, Lushoto, Same, Mbulu, Msalala na Mpanda. Halmashauri nyingine ni Maswa, Songea Vijijini, Rufiji, Karatu na Kwimba. Vilevile, imejenga maghala matano yenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000 za mazao kila moja katika halmashauri za Iringa Vijijini, Njombe Vijijini, Same, Songea na Mbarali na kukarabati maghala matatu katika Halmashauri za Sumbawanga, Mbulu na Kahama. Aidha, Programu hiyo imezijengea uwezo benki tisa za wananchi/ushirika ili kuimarisha mfumo wa kifedha Vijijini.
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Programu hiyo imepanga kukarabati kilometa 434 za barabara kwa kiwango cha changarawe, kujenga maghala 14 na masoko saba katika Halmashauri 64 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar. Aidha, wazalishaji wadogo kutoka Mikoa 24 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar watajengewa uwezo wa kuhifadhi mazao na mbinu za kufikia masoko ambapo zaidi ya wananchi 100,000 watanufaika na mafunzo hayo.
48. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013 imetungwa na imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo itawezesha kuanzishwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo itakuwa na majukumu ya kusimamia moja kwa moja Vyama vyote vya Ushirika. Aidha, kupitia Sheria hiyo, Serikali imetoa Waraka Namba 1 wa mwaka 2014 unaotoa ufafanuzi kuhusu Chaguzi katika Vyama vya Ushirika. Ili kuondoa migogoro ya kimaslahi, Waraka huo umewaondoa Viongozi wa Siasa na Serikali katika uongozi wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaimarisha uratibu wa Vyama vya Ushirika kulingana na mahitaji ya Wananchi na kuunganisha Vyama vya Ushirika na Taasisi za fedha ili kuboresha utoaji wa huduma za kifedha kwa Vyama vya Ushirika.
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo
49. Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Ruzuku ya dawa ya kuogeshea mifugo, Serikali ilitoa jumla ya lita 11,020 zenye thamani ya Shilingi Milioni 181.8 na kusambazwa nchini. Vilevile, ilitoa chanjo kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo ambapo dozi 150,000 za chanjo ya Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa zenye thamani ya Shilingi milioni 119 ilitolewa katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Dodoma. Vilevile, Serikali imeimarisha Kituo cha Uhamilishaji kilichopo katika eneo la Usa River, Arusha pamoja na Vituo vingine vitano vya Kanda kwa kusimika mitambo ya kuzalisha kimiminika cha naitrojeni na kujenga Vituo vitano vya madume bora. Vilevile, ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kutoka 132,246 mwaka 2011/2012 hadi kufikia 175,000 mwaka 2013/2014. Ili kuboresha upatikanaji wa maziwa Nchini, Serikali imeongeza uzalishaji mitamba katika mashamba yake kutoka mitamba 943 kwa mwaka 2012/2013 hadi mitamba 1,046 mwaka 2013/2014 na kusambaza Mbuzi wa maziwa 9,530 kupitia Mpango wa Kopa Mbuzi lipa Mbuzi. Jitihada hizi, zimesaidia wafugaji kuongeza tija na hivyo kuchangia ongezeko la uzalishaji wa maziwa kutoka lita Bilioni 1.9 mwaka 2012/2013 hadi lita Bilioni 2 mwaka 2013/2014.
50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa ruzuku ya dawa za kuogesha mifugo na kununua dozi milioni moja kwa ajili ya chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa kwa Mikoa ya Arusha, Tanga, Tabora na baadhi ya mikoa katika Kanda ya Ziwa. Vilevile, Serikali itaimarisha Vituo vya uhamilishaji, mashamba ya kuzalisha mifugo bora na yale yanayozalisha mbegu bora za mifugo pamoja na kununua mifugo wazazi.
51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na wadau ilihuisha Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia. Katika kuimarisha ufugaji wa samaki, wakulima 2,604 walipewa mafunzo ya ufugaji bora wa samaki na mabwawa 64 yalichimbwa. Hatua hiyo imeongeza idadi ya mabwawa ya Samaki kufikia 20,198 yenye uwezo wa kuzalisha Tani 3,029.7 za samaki ikilinganishwa na mabwawa 20,134 yaliyokuwepo mwaka 2012/2013. Vituo vya kuzalisha vifaranga wa samaki kwa wingi kwa kutumia teknolojia ya ndani viliongezeka kutoka kituo kimoja mwaka 2012/2013 hadi kufikia vituo vitano mwaka 2013/2014 vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga bora vya samaki Milioni 10 kwa mwaka. Serikali pia, ilijenga matanki sita yenye lita za ujazo 8,000 kila kimoja kwa ajili ya kuzalisha vifaranga vya samaki.
52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanzisha Vituo vya kuzalishia vifaranga vya samaki katika maeneo ya Bacho Dareda - Manyara, Hombolo – Dodoma, na Kigoma. Vilevile, itajenga bwawa la kufuga samaki katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro – KATC; na kutoa ruzuku kwa ajili ya kuchimba mabwawa na kuzalisha vifaranga wa samaki.
Ufugaji Nyuki
53. Mheshimiwa Spika, Sekta ya ufugaji nyuki imeendelea kuimarika na kuchangia kuongeza ajira na kupunguza umaskini. Mwaka 2013, thamani ya mauzo ya asali nje yalifikia Shilingi Milioni 287.3 ikilinganishwa na mauzo ya Shilingi Milioni 262 mwaka 2012. Katika kipindi hicho, jumla ya Tani 384 za nta zenye thamani ya Shilingi Milioni 4,660 ziliuzwa nje ikilinganishwa na Tani 277 zenye thamani ya Shilingi Milioni 2,583 zilizouzwa mwaka 2012. Nchi zilizoongoza katika ununuzi wa Asali na Nta ya Tanzania ni Ujerumani, Oman, China, Japan, Yemen, India, Ubelgiji, Botswana, Kenya na Marekani. Kutokana na maendeleo haya mazuri katika mwaka 2013/2014, Serikali imetenga maeneo 20 yenye ukubwa wa Hekta 58,445 sehemu mbalimbali Nchini kwa ajili ya hifadhi za nyuki. Aidha, imetoamafunzo kwa wafugaji nyuki 924 na vikundi 49 kutoka Wilaya 12 pamoja na kutoa elimu ya miongozo na sheria za ubora wa mazao ya nyuki kwa wafanyabiashara wa mazao ya nyuki.
54. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tanzania ilishiriki kwenye Kongamano la Ufugaji nyuki lililofanyika Kiev, Ukraine. Katika Kongamano hilo, mazao ya nyuki kutoka Tanzania yalikuwa kivutio kikubwa na yaliwezesha kupata medali ya Banda Bora la Asali kutokana na asali yake kuwa na viwango vya ubora na usalama vinavyokubalika Kimataifa. Aidha, kampuni mbalimbali zilionesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya ufugaji nyuki Nchini. Kama ambavyo nimesisitiza mara kwa mara, sekta ya nyuki ina fursa kubwa ya kibiashara hapa nchini na nje ya nchi. Ni sekta inayoweza kuleta mapinduzi makubwa katika maeneo mengi kwani yanahitajika mafunzo kidogo na vifaa vichache ambavyo vinaweza kutumika kikamilifu kupata asali na mazao yake. Niendelee kusisitiza kwamba, tuwahimize wananchi katika Majimbo yetu watumie fursa za ufugaji nyuki zinazopatikana katika maeneo yao ili kujiongezea kipato.
Maendeleo ya Viwanda
55. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo imeendelea kutoa mchango muhimu katika upatikanaji wa ajira, ongezeko la kipato na ukuaji wa uchumi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imefungua Vituo vya Teknolojia Mikoani kwa ajili kuhudumia Wajasiriamali wanaotengeneza mashine za kusindika mazao na kutengeneza bidhaa mbalimbali za uzalishaji mali. Vituo hivyo vimewezesha kuanzishwa kwa miradi mipya 4,127 ya uzalishaji mali kwenye mikoa ya Lindi, Mbeya, Iringa, Arusha, Kigoma na Kilimanjaro. Aidha, Wajasiriamali 23,546 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi maalum wa ufundi na utumiaji wa mashine za uzalishaji mali. Vilevile, huduma za ushauri na ugani zilitolewa kwa Wajasiriamali 20,769 kwenye Vikundi na Vyama vyao vya Biashara kwa kuviimarisha na kuviwezesha kujenga misingi ya kujitegemea.
56. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mkakati wa “Wilaya Moja, Bidhaa Moja” kwa kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa kutokana na malighafi zilizopo kwenye Wilaya husika. Kupitia Mkakati huo, Serikali imejenga uwezo wa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali, kuzalisha mitambo na vipuri pamoja na zana za kilimo ambapo viwanda vidogo 198 vilianzishwa na kuwezesha upatikaji wa ajira 1,809. Aidha, Serikali inatekeleza Mradi wa Kuendeleza Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwa kutumia dhana ya kuimarisha mlolongo wa thamani kimikoa kwa mazao mbalimbali. Mradi umewezesha uanzishwaji wa miradi midogo 15,580 Vijijini; urasimishaji wa Vikundi 65,308 vya uzalishaji na upatikanaji wa ajira 39,574.
57. Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea na juhudi za kuhamasisha uwekezaji kwenye miradi mipya katika Maeneo Maalum ya Uzalishaji (Export Processing Zones) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Special Economic Zones). Hadi kufikia mwezi Desemba 2013, kampuni 32 zilikuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya EPZ kwa ajili ya kuanzisha viwanda vipya kwenye maeneo hayo. Aidha, Serikali imekamilisha utafiti kwenye Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na kuthibitisha uwepo wa tani Milioni 370 za makaa ya mawe katika eneo la kilomita za mraba 30 kati ya kilomita za mraba 140 zilizotengwa kwa ajili ya Mradi huo. Aidha, utafiti huo ulithibitisha uwepo wa tani Milioni